21 wahukumiwa kifungo cha maisha jela Burundi kwa 'kupanga mapinduzi'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i6781-21_wahukumiwa_kifungo_cha_maisha_jela_burundi_kwa_'kupanga_mapinduzi'
Mahakama ya Juu ya Burundi imetoa hukumu ya maisha jela kwa maafisa 21 wa jeshi la nchi hiyo, wanaodaiwa kuhusika na njama iliyofeli ya kuipindua serikali mwezi Mei mwaka jana wa 2015.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 10, 2016 02:25 UTC
  • 21 wahukumiwa kifungo cha maisha jela Burundi kwa 'kupanga mapinduzi'

Mahakama ya Juu ya Burundi imetoa hukumu ya maisha jela kwa maafisa 21 wa jeshi la nchi hiyo, wanaodaiwa kuhusika na njama iliyofeli ya kuipindua serikali mwezi Mei mwaka jana wa 2015.

Duru za habari kutoka mji wa Gitega eneo la kati kati mwa nchi zinasema kuwa, hukumu hiyo ilitolewa jana Jumatatu na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo na miongoni mwa askari waliohukumiwa ni Jenerali Cyrille Ndayirukiye, kamanda mwandamizi wa jeshi la nchi hiyo. Mwezi Januari mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela kwa maafisa 9 wa jeshi la nchi hiyo na kifungo cha miaka 5 jela kwa wanajeshi wengine waliotuhumiwa kuhusika na njama ya kuipindua serikali ya Rais Pierre Nkurunziza.

Hii ni katika hali ambayo, machafuko na mauaji yanaendelea kushuhudiwa nchini humo. Taarifa iliyotangazwa jana na polisi ya nchi hiyo ilisema kuwa, mashambulizi ya maguruneti yaliyoanza tangu siku ya Ijumaa mjini Bujumbura hadi sasa yamesababisha kwa akali watu watatu kuuawa na wengine 20 kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 400 wameuawa na wengine karibu laki mbili na 60 elfu wamekuwa wakimbizi tangu nchi hiyo ilipotumbukia katika machafuko mwanzoni mwa mwaka jana, kufuatia hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kutangazwa na chama chake cha CNDD-FDD kugombea kwa muhula wa tatu katika uchaguzi mkuu uliopita.