Watu 30 wauliwa katika shambulizi la silaha, nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i68542-watu_30_wauliwa_katika_shambulizi_la_silaha_nchini_ethiopia
Watu waliokuwa na bunduki wamewauwa raia wasiopungua 30 katika shambulio lililolenga kijiji kimoja katika mkoa wa Oromia nchini Ethiopia. Shambulizi hilo linatambuliwa kuwa ni katika mfululizo wa ghasia za kikabila za hivi karibuni za wapinzani wa serikali ya shirikisho.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Apr 01, 2021 03:46 UTC
  • Watu 30 wauliwa katika shambulizi la silaha, nchini Ethiopia

Watu waliokuwa na bunduki wamewauwa raia wasiopungua 30 katika shambulio lililolenga kijiji kimoja katika mkoa wa Oromia nchini Ethiopia. Shambulizi hilo linatambuliwa kuwa ni katika mfululizo wa ghasia za kikabila za hivi karibuni za wapinzani wa serikali ya shirikisho.

Watu walioshuhudia wanasema, maiti za watu wasiopungua 30 ziliokotwa na kuzikwa jana baada ya watu waliokuwa na silaha kushambulia eneo la Wollega mkoani Orumia na kwamba shambulizi hilo lililenga watu wa kabila la Amhara.

Wakazi wa wilaya ya Babo-Gembel ambako shambulio hilo lilitokea, wamewaambia waandishi habari kwamba watu waliokuwa na silaha walifika eneo hilo saa 9 alasiri na kuwalazimisha wakaazi kukusanyika nje kwenye kundi na kisha wakawapiga risasi na kuwaua.

Mamlaka za eneo hilo zimelihusisha shambulio hilo, ambalo pia limejeruhi watu wengine 15, na kikundi lililojitenga kutoka Oromo Liberation Front (OLF). OLF ni chama cha upinzani ambacho kilikuwa uhamishoni kwa miaka mingi lakini kiliruhusiwa tena kufanya shughuli zake nchini Ethiopia baada ya Waziri Mkuu wa sasa wa nchi hiyo, Abiy Ahmed kuchukua madaraka mwaka 2018.

Oromo ndio kabila kubwa zaidi nchini Ethiopia likifuatiwa na kabila la Amhara. Mikoa miwili jirani ya Amhara na Oromia inashirikiana mpaka. Raia kutoka kabila moja wanaoishi upande wa pili wa mpaka wamekuwa wakishambuliwa mara kwa mara na mahasimu wao katika miezi ya hivi karibuni.

Machafuko ya kikabila Ethiopia

Mwenyekiti wa Chama cha Amhara Association of America kilichoko Washington, DC, Tewodrose Tirfe, amesema zaidi ya watu 300 wa kabila la Amhara wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa na Jeshi la Ukombozi wa Oromo katika mwezi uliopita wa Machi.

Tirfe ameituhumu serikali ya Ethiopia kuwa "imenyamazia kimya" mauaji hayo.