Apr 13, 2021 13:42 UTC
  • Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi
    Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi

Kamati za Bunge la Kenya zimetuhumiwa kuwa zinakula rushwa na kuhusika na ufisadi kutokana na wabunge wanaosimamia kamati hizo kufumbia macho uhalifu na mashtaka yanayowasishwa mkabala wa kula rushwa na kupokea hongo.

Huku Spika wa Bunge la Kenya, Justin Muturi akiahidi kuwa madai ya ufisadi yaliyotolewa dhidi ya baadhi ya wabunge na kampuni moja ya kutengeneza mvinyo yatachunguzwa, imebainika kuwa wabunge hutumia kamati zao kama majukwaa ya kujitajirisha kinyume cha sheria.

Spika Muturi amethibitisha kupokea barua kutoka kwa mwenyekiti wa kampuni ya London Distiller Kenya Ltd (LDK) Mohan Galot, akilalamika kuwa wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji walihongwa na kampuni ya nyumba ya Erdermann Property Ltd ili wapendekeze kufungwa kwake.

Kampuni hiyo inayomiliki mtaa wa makazi ya Great Wall Garden iliyoko Athi River nje kidogo ya jiji la Nairobi ilidai kuwa, kampuni ya LDK imekuwa ikiachilia maji taka katika mto Athi na hivyo kuhatarisha maisha ya wakazi. Madai hayo yalichunguzwa na Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira na Mali Asili ambayo ilipendekeza kampuni ya LDK ifungwe ikiwa haitasita kuachilia maji taka katika mto Athi.

Katika barua yake kwa Muturi Bw Galot anasema: “Wabunge wanachama wa kamati hiyo walipewa nyumba bila malipo au kwa bei nafuu kupitia jamaa zao au kampuni ambazo wao ni wakurugenzi ili wapendekeze kufungwa kwa LDK.

Madai ya ufisadi dhidi ya wanachama wa Kamati ya Bunge la Kenya kuhusu Utekelezaji ni mojawapo tu ya msusuru wa madai kama hayo ambayo yameshusha hadhi ya Bunge.

Bunge la Kenya

Wabunge wa Kenya wamekuwa wakikashifiwa kwa kupokea mamilioni ya fedha ili kuwakinga maafisa wa umma wanaofika mbele ya kamati zao kuchunguzwa kuhusiana na tuhuma mbalimbali za ufisadi na uhalifu wa kifedha.

Wabunge wanachama wa kamati ambazo huchunguza ripoti za Mkaguzi wa Hesabu za Serikali zinazofichua visa mbalimbali vya matumizi mabaya ya fedha za umma katika asasi za serikali na serikali za kaunti wameshutumiwa kupokea hongo ili kuwalinda maafisa husika au kuandika ripoti inayowaondolea lawama.

Vilevile, kumekuwa na madai ya wabunge kuhongwa ili kutupilia mbali ripoti ya kamati za Bunge zinazopendekeza maafisa wakuu wa serikali kuchukuliwa hatua za kisheria.

Tags