Macron akiri, Ufaransa ilihusika katika mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994
Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amekiri kwamba, nchi yake ilihusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
Macron ambaye jana Alkhamisi alikuwa akizungumza mjini Kigali nchini Rwanda amesema kuwa: "Nawaomba radhi kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Ufaransa ilikuwa na mchango katika mauaji ya kimbari ya Rwanda na ina makosa katika uwanja huu."
Macron ni Rais wa kwanza wa Ufaransa kuitembelea Rwanda tangu mwaka 2010.
Rwanda inaituhumu Ufaransa kwamba, ilihusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994. Hata hivyo katika safari yake ya karibuni nchini Ufaransa, Rais Paul Kagame wa Rwanda alisema: "Sasa umewadia wakati wa kuisamehe Ufaransa kutokana na mauaji ya kimbari yaliyofanywa dhidi ya Watutsi."
Hatua ya Rais Emmanuel Macron ya kukiri kwamba, Ufaransa ilihusika katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi miaka 27 sasa tangu baada ya maafa hayo makubwa yaliyosababisha mauaji ya karibu wanadamu milioni moja, ni kielelezo kingine cha jinsi Wamagharibi wasivyojali misingi ya ubinadamu na jinsi nchi hizo zinavyojaribu kuficha na kukwepa majukumu yao ya kuhusika katika jinai na ukatili zinaoufanya katika mataifa mengine hususan barani Afrika. Awali Macron pia alilazimika kukiri kwamba, Ufaransa ilihusika katika jinai na mauaji ya Waalgeria. Raia milioni moja wa Algeria waliuawa kwa umati na askari wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa baina ya mwaka 1945 na 1962. Hata hivyo Macron hakuwa tayari kuomba radhi kutokana na mauaji hayo.

Faili la jinai kubwa na za kutisha za Ufaransa ambayo inadai kutetea uhuru na haki za binadamu na kuhusika kwake katika mauaji ya mamilioni ya Waalgeria na Wanyarwanda ni kubwa sana kiasi kwamba, jinai hiyo haiwezi kuhalalishwa au kufichika. Matokeo ya uchunguzi uliofanyika mwaka 2017 kwa maagizo ya serikali ya Rwanda yalibaini kuwa, serikali ya Ufaransa ilishirikiana na Wahutu wenye misimamo mikali katika mauaji ya Watutsi zaidi ya laki nane. Uchunguzi huo uliokusanywa kwenye kurasa karibu mia sita unasisitiza kuwa, Ufaransa ilikuwa na taarifa kamili kuhusu mipango ya mauaji ya kimbari ya Rwanda. Kampuni ya Levy Firestone Muse LLP iliyotayarisha ripoti hiyo inasema kuwa, Ufaransa ilihusika pakubwa katika mauaji hayo ya kimbari. Kampuni hiyo imepata ripoti na taarifa hizo kutoka kwenye mamilioni ya nyaraka na mahojiano iliyofanya na zaidi ya watu 250.
Vilevile matokeo mengine ya utafiti wa tume ya uchunguzi ya Ufaransa kuhusu nafasi ya nchi hiyo katika mauaji ya kimbari ya Rwanda yanaonesha kuwa, japokuwa Paris haikushiriki moja kwa moja katika mauaji ya mwaka 1994 nchini Rwanda, lakini inabeba majukumu mazito kuhusiana na mauaji hayo. Ripoti ya tume hiyo liyotayarishwa kutokana na nyaraka elfu nane za Ofisi ya Rais na Waziri Mkuu wa Ufaransa kuhusiana na kadhia hiyo inadai kuwa, Ufaransa haikushiriki lakini ilipanga mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.
Uchunguzi huo unasema kuwa, serikali ya wakati huo ya Ufaransa iliyokuwa ikiongozwa na François Mitterrand ilikuwa na mchango mkubwa katika mauaji ya watu laki nane nchini Rwanda aghlabu yao wakiwa wa kabila la Tutsi.
Sambamba na kudai kuwa Ufaransa haikushiriki moja kwa moja katika mauaji hayo ya kimbari dhidi ya Watutsi, lakini uchunguzi huo unasisitiza kuwa, Paris inabeba lawama kubwa na ilikuwa na mchango muhimu sana katika jinai hiyo, hasa kwa kutilia maanani uhusiano wa karibu sana uliokuwepo baina ya Ufaransa na serikali ya wakati huo ya Rwanda, misaada ya Paris ya kuwatorosha watuhumiwa wa mauaji hayo waliokuwa wakipewa himaya na jeshi la Ufaransa na nafasi yake katika kikosi cha wanaeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Rwanda.

Mtafiti wa Kifaransa, Francois Graner anasema: "Nyaraka zote zinazohifadhiwa katika makavazi zinaonesha kuwa, Ufaransa iliwaunga mkono na kuwasaidia Wahutu. Maafisa wa serikali ya Ufaransa walijulishwa kwamba, Wahutu wanajitayarisha kwa ajili ya mauaji ya kimbari. Paris iliwaunga mkono na kuwasaidia Wahutu hao wakati wote wa kabla na baada ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi."
Swali linalojitokeza hapa ni kwamba, je kukiri kwa maneno tu Rais Emmanuel Macron kwamba Ufaransa ilihusika katika mauaji ya kimbari ya karibu watu milioni moja nchini Rwanda kunatosha, au kuna udharura wa viongozi na maafisa wa Ufaransa waliohusika katika maafa hayo makubwa wafuatiliwe na kufikishwa mahakamani?