Jun 02, 2021 02:28 UTC
  • Kuendelea harakati za magaidi nchini Nigeria; wanafunzi 200 watekwa nyara

Makundi ya kigaidi katika eneo la Afrika Magharibi hasa nchini Nigeria yamekithirisha vitendo vya uhalifu, na katika tukio la hivi karibuni wanafunzi karibu 200 wa shule moja ya Kiislamu wametekwa nyara kati mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jumatatu ya msemaji wa polisi ya Nigeria, Wasiu Abiodun, wanafunzi karibu 200 wa shule ya Kiislamu ya Salihu Tanko eneo la Rafi katika jimbo Niger walitekwa nyara na watu ambao walikuwa wakifyatua risasi kiholela. Katika tukio hilo mtu mmoja aliuawa.

Katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, makundi ya magaidi waliojizatiti kwa silaha wameshambulia shule na kuwateka nyara wanafunzi. Takwimu zinaonesha kuwa, tangu Disemba 2020 hadi sasa zaidi ya wanafunzi 700 wametekwa nyara na magaidi nchini Nigeria. Baadhi wameachiliwa huru baada ya vikomboleo kulipwa na wengine wameokolewa katika oparesheni za maafisa wa usalama.

Utekaji nyara wanafunzi umeshadidi Nigeria katika hali ambayo serikali ya nchi hiyo inadai kuwa, moja ya vipaumbele vyake muhimu ni kupambana na makundi ya kigaidi hasa kundi la kigaidi la Boko Haram. Hivyo kuongezeka hujuma za kigaidi nchini Nigeria ni ushahidi wa wazi kwamba serikali ya nchi hiyo imeshindwa katika kukabiliana na magaidi.

Inaonekana kuwa, kundi la Boko Haram linawashambulia na kuwateka nyara wanafunzi kwa malengo kadhaa ikiwa ni pamoja na kuibuwa wahka na woga katika jamii, kuongeza idadi wa wapiganaji wake na pia kwa ajili ya pato. Watekaji nyara huwa wanataka kiasi kikubwa cha fedha kama kikomboleo kabla ya kuwaachilia huru wanafunzi waliotekwa nyara. Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Nigeria hadi sasa familia za wanafunzi waliotekwa nyara zimetoa Naira milioni 180 au Euro karibu laki 357 ili watoto wao waachiliwe huru.

Aidha duru zinadokeza kuwa, idadi kubwa ya wanafunzi waliotekwa nyara wanalazimishwa kupata mafunzo ya kijeshi na wanatumiwa katika oparesheni za kigaidi, na hata wengine wamepoteza maisha katika oparesheni za kujirupua kwa mabomu.

Weledi wa mambo wanasema kuwa, sababu ya kushadidi harakati za kigaidi nchini Nigeria ni pamoja na hali mbaya ya kiuchumi, kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira, umasikini mkubwa, sera za ukandamizaji na uingiliaji wa madola ya kigeni. Hali ni mbaya kiasi kwamba baadhi ya ripoti zinasema, baadhi ya wanavijiji wanashirikiana na watekaji nyara kwa ajili ya fedha wanazopata.

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria

Kwa hivyo ingawa kundi la Boko Haram limedai kuhusika na hujuma za kigaidi lakini ushahidi unaonyesha kuwa, wanafunzi waliotekwa nyara wanashikiliwa na makundi ya wahalifu na hivyo kinachofanyika ni kuwa Boko Haram inaunda muungano na makundi hayo ya wahalifu. Hivyo magaidi na wahalifu wanatumia vibaya hali ya umasikini kujipenyeza vijijini. Ni kwa msingi huo ndio maana Waziri wa Usalama wa Nigeria, Lai Mohammad akasema Boko Haram inadai kuhusika na utekaji nyara ili kuoneysha kuwa bado ni kundi lenye nguvu na uwezo, ilhali wanafunzi waliotekwa nyara wanashikiliwa na magenge ya wahalifu.

Pamoja na hayo maudhui asili si swala la kuhusika Boko Haram au la, bali ni kumeongezeka utekaji nyara wanafunzi sambamba na kushadidi oparesheni za kigaidi katika maeneo mbalimbali ya Nigeria. Ugaidi huo umeongezeka licha ya kuwa serikali ya Nigeria inadai kushirikiana na nchi za Magharibi hasa Marekani katika kuangamiza magaidi, lakini si tu kuwa magaidi hawajapungua bali harakati zao, hasa za Boko Haram, zimepamba moto zaidi.

Tags