Rais wa Afrika Kusini apasisha kumiminwa mitaani askari 25,000 kudhibiti ghasia
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameidhinisha kumiminwa mitaani askari 25,000 ili kudhibiti ghasia zilizozuka baada ya kufungwa jela rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.
Kabla ya hapo habari zilikuwa zimesema kuwa, Serikali ya Afrika Kusini imekusudia kumimina askari 25,000 mitaani kama sehemu ya hatua mpya za kudhibiti machafuko yanayoitesa nchi hiyo kwa siku kadhaa sasa huku kukiwa na hofu ya upungufu wa chakula na mafuta.
Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini alikuwa amesema bungeni kwamba kuna wajibu wa kutumwa mitaani askari 25,000 wa kukabiliana na fujo, lakini jambo hilo haliwezi kufanyika bila ya idhini ya Rais Cyril Ramaphosa wa nchi hiyo.
Jana Alkhamisi pia, vyombo vya habari vilinukuu serikali ya Afrika Kusini ikisema kuwa, siku ya Jumatano kulitokea vitendo 208 vya uporaji licha ya idadi ya askari wa kuzuia fujo kuongezwa mitaani.
Sekta ya uchukuzi na usafirishaji hasa katika jimbo la KwaZulu Natal huko kusini mashariki mwa Afrika Kusini imeathiriwa vibaya na wizi na hilo litaathiri moja kwa moja zoezi zima la kusambaza chakula na kutoa huduma katika kona zote za Afrika Kusini.
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika ghasia zinazoendelea nchini humo imepindukia 117 huku mamia wakitiwa mbaroni wakihusishwa na vurugu hizo.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametoa mwito kwa Waafrika Kusini kuzingatia athari mbaya za vitendo vyao na machafuko ya sasa nchini humo.
Wiki iliyopita Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini iliagiza Rais mstaafu wa nchi hiyo, Jacob Zuma afungwe jela kwa kukataa kutoa ushahidi katika uchunguzi wa ufisadi uliofanyika wakati wa uongozi wake kuanzia mwaka 2009 hadi 2018.