Upinzani nchini Afrika Kusini wataka Jacob Zuma arudishwe jela
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i74520-upinzani_nchini_afrika_kusini_wataka_jacob_zuma_arudishwe_jela
Upinzani nchini Afrika Kusini umewasilisha malalamiko mahakamani ukitaka rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma arejeshwe gerezani.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Sep 11, 2021 03:01 UTC
  • Upinzani nchini Afrika Kusini wataka Jacob Zuma arudishwe jela

Upinzani nchini Afrika Kusini umewasilisha malalamiko mahakamani ukitaka rais wa zamani wa nchi hiyo Jacob Zuma arejeshwe gerezani.

Zuma, aliyefungwa jela tangu mapema mwezi Julai kwa kudharau mahakama, aliachiliwa Jumapili, Septemba 5, kwa kile kilichotajwa kuwa ni sababu za matibabu. Mamlaka ya magereza ilimuachilia kwa dhamana, hata hivyo upinzani umepaza sauti na kulaani uamuzi huo ambao umeutaja kuwa wa kisiasa.

Chama kikuu cha upinzani, Democratic Alliance, kimesema, kuachiliwa kwa Jacob Zuma ni kinyume cha sheria. Uamuzi wa mwisho wa kumwachilia Jacob Zuma ulichukuliwa na Kamishna wa mamlaka ya magereza, Arthur Frazer. Kutokana na hatua hiyo upiinzani umetaka kujua ni nini kilichopelekea kuchukuliwa kwa uamuzi huo.

Arthur Frazer

Katika taarifa, mamlaka ya magereza nchini Afrika Kusini imeeleza kuwa uamuzi huo ulichukuliwa kulingana na "ripoti ya matibabu", lakini bila kutoa maelezo zaidi. Mwezi uliopita, Jacob Zuma alifanyiwa upasuaji, ambao sababu yake haijabainishwa.

Hata hivyo chama cha Democratic Alliance kimetilia shaka uhusiano uliopo kati ya Jacob Zuma na Arthur Frazer.

Itakumbukwa kuwa Arthur Frazer aliteuliwa na Jacob Zuma mwenyewe alipokuwa rais kuwa mkurugenzi mkuu wa idara ya ujasusi, miaka mitano iliyopita.../