Wafungwa wa Misri wasusia chakula kukosoa 'kesi bandia'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i7672-wafungwa_wa_misri_wasusia_chakula_kukosoa_'kesi_bandia'
Makumi ya wafungwa wa Misri walioshiriki maandamano ya kuikosoa serikali ya Cairo kwa kuipa Saudi Arabia visiwa viwili vinavyomilikiwa na nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wanafanya mgomo wa kula, kulalamikia kile walichokitaja kuwa kesi bandia na za kidhulma dhidi yao.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 23, 2016 12:17 UTC
  • Wafungwa wa Misri wasusia chakula kukosoa 'kesi bandia'

Makumi ya wafungwa wa Misri walioshiriki maandamano ya kuikosoa serikali ya Cairo kwa kuipa Saudi Arabia visiwa viwili vinavyomilikiwa na nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wanafanya mgomo wa kula, kulalamikia kile walichokitaja kuwa kesi bandia na za kidhulma dhidi yao.

Mokhtar Mounir, mmoja wa mawakili wa wafungwa hao amesema hatua ya wafungwa hao kususia chakula chini ya mazingira magumu ya jela inaashiria namna walivyoghadhabishwa na kesi dhidi yao kwa kushiriki katika zoezi la kidemokrasia kukosoa 'uhuni' wa serikali. Naye Misr Abdel-Wahed, dada ya mmoja wa wafungwa hao amewaambia waandishi wa habari kuwa, wafungwa watatu miongoni mwa wanaofanya mgomo wa kula wako katika hali mbaya hospitalini na kwamba walianza kususia chakula juma lililopita.

Mei 15, mahakama moja nchini Misri iliwahukumu watu 152 kifungo cha kati ya miaka miwili hadi mitano jela kwa kushiriki maandamano ya Aprili 25 ya kupinga hatua ya serikali ya nchi hiyo kuipa Saudi Arabia visiwa viwili, vinavyomilikiwa na nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch lilisema hivi karibuni kwamba vyombo vya usalama vya Misri viliwakamata waandamanaji 382, walioshiriki maandamano hayo ya mwezi jana, ya kupinga hatua ya Rais Abdul Fattah al-Sisi wa nchi hiyo, kuipa Saudi Arabia visiwa viwili vya Misri vya Sanafir na Tiran.

Iliarifiwa kuwa, serikali ya Misri ilipokea dola bilioni 20 za Marekani kutoka utawala wa Aal-Saud ili kuuzia visiwa hivyo, ambavyo ni milki ya nchi hiyo ya Kiafrika.