Moto uliochoma Bunge Afrika Kusini, Ramaphosa atoa amri ya kufanyika uchunguzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i78768-moto_uliochoma_bunge_afrika_kusini_ramaphosa_atoa_amri_ya_kufanyika_uchunguzi
Rais wa Afrika Kusini ametoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina na wa haraka baada ya jengo la Bunge la nchi hiyo kuteketea kikamilifu kwa moto mjini Cape Town. Jengo hilo lina umri wa miaka 138.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 03, 2022 04:09 UTC
  • Moto uliochoma Bunge Afrika Kusini, Ramaphosa atoa amri ya kufanyika uchunguzi

Rais wa Afrika Kusini ametoa amri ya kufanyika uchunguzi wa kina na wa haraka baada ya jengo la Bunge la nchi hiyo kuteketea kikamilifu kwa moto mjini Cape Town. Jengo hilo lina umri wa miaka 138.

Rais Cyril Ramaphosa alitoa amri hiyo jana Jumapili na kusema kwamba anaamin kuna mtu anashikiliwa kwa usaili kuhusu moto huo uliotokea mapema jana alfajiri.

Kabla ya hapo msemaji wa Bunge la Afrika Kusini alikuwa ametoa taarifa rasmi ya kutokea moto mkubwa ulioteketeza kikamilifu jengo la Bunge mjini Cape Town.

Moto huo ulitokea saa 11 alfajiri jana Jumapili kwa wakati wa Afrika Kusini masaa machache baada ya kufanyika kumbukumbu maalumu za kumuenzi Askofu Desmond Tutu, mpigania ukombozi wa Afrika Kusini aliyefariki dunia hivi karibuni. 

Moshi mzito ukitoka kwenye jengo la Bunge la Afrika Kusini mjini Cape Town

Katika ujumbe wake kwa vyombo vya habari, Rais Ramaphosa amesema: "Tunahitaji kufanya uchunguzi wa kina wa kugundua tukio hili lilivyotokea na hatua gani tunapaswa kuzichukua."

Amesema, moto huo ulianzia kwenye ukumbi wa jengo la zamani na baadaye ukaenea maeneo mengine ya jengo hilo.

Rais Ramaphosa vile vile amesema, amewaomba maafisa wa ngazi za juu kuelekea haraka mjini Cape Town kukabiliana na tukio hilo akiwemo Spika wa Bunge la Taifa, Nosiviwe Mapisa-Nqakula.

Hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa katika tukio hilo kwani vikao vya bunge vimefungwa kutokana na mapumziko ya mwaka mpya wa Milaadia.

Jeshi la Polisi la Afrika Kusini kupitia Brigedia Nomthandazo Mbambo limesema kuwa, mtu aliyetiwa mbaroni atapandishwa kizimbani kwa tuhuma za kushambulia maeneo muhimu ya kiistratijia. Hata hivyo amesema, maelezo zaidi yatatolewa baadaye.