Askari polisi wanne wa Kenya wauawa, magaidi wa Ash-Shabaab washukiwa kuhusika
(last modified Sat, 08 Jan 2022 03:24:48 GMT )
Jan 08, 2022 03:24 UTC
  • Askari polisi wanne wa Kenya wauawa, magaidi wa Ash-Shabaab washukiwa kuhusika

Maafisa wanne wa polisi ya Kenya wameuawa katika shambulio la kuvizia katika eneo la pwani ya nchi hiyo linalopakana na Somalia, amblo hulengwa mara kwa mara na wanamgambo wa kundi la kigaidi la Ash-Shabaab.

Shambulizi hilo lilitokea jana katika Kaunti ya Lamu, takriban kilomita 420 kutoka mji mkuu Nairobi, ambapo serikali ilikuwa imetuma vikosi vya usalama na kutangaza sheria ya kutotoka nje usiku baada ya mauaji ya raia saba katika mashambulizi mawili mapema wiki hii.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu Irungu Macharia amethibitisha vifo vya askari hao na kueleza kwamba, gari lao lilishambuliwa kwa roketi na kushika moto.

Kwa upande wa jeshi la Polisi la Kenya, japokuwa limethibitisha kwamba askari wake waliokuwa wakishika doria mapema asubuhi jana wameshambuliwa, lakini haikutoa ripoti sahihi.

Kaunti ya Lamu, iko karibu na mpaka na Somalia na imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi kadhaa ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Ash-Shabaab.

Wanamgambo wa kundi la kigaidi la Ash-Shabaab

Tangu Kenya ilipotuma vikosi vya jeshi lake nchini Somalia mwaka wa 2011 kupambana na wanamgambo wa Ash-Shabaab, imelengwa na mashambulizi kadhaa mabaya ya kundi hilo kigaidi na ukufurishaji, likiwemo la mwezi Septemba 2013 dhidi ya kituo cha biashara cha Westgate mjini Nairobi ambalo lilisababisha vifo vya watu 67, na la Aprili 2015 dhidi ya Chuo Kikuu cha Garissa mashariki mwa nchi hiyo ambapo watu 148 waliuawa.

Mapema wiki hii, polisi iliwahusisha magaidi wa Ash-Shabaab na mauaji ya raia saba huko Lamu.

Mtu mmoja alikatwa kichwa na wengine kupigwa risasi au kuchomwa moto wakiwa hai katika mashambulizi mawili tofauti siku ya Jumapili na Jumatatu. Lakini mamlaka za serikali baadaye zilisema ghasia hizo zilisababishwa na mzozo wa ardhi katika eneo hilo.../

 

 

Tags