Jan 13, 2022 04:21 UTC
  • Vita vya Ethiopia na jitihada za kutatua mgogoro wa nchi hiyo

Wakati maafisa wa serikali ya Ethiopia wakiahidi kuanzisha mazungumzo ya kitaifa nchini humo, Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) imetangaza kuwa mashambulizi ya jeshi la Ethiopia katika eneo hilo yamesababisha vifo vya zaidi ya raia 56.

Kuhusiana na suala hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameeleza kusikitishwa na mauaji ya raia katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia na kutoa wito wa kusitishwa mara moja mzozo wa nchi hiyo.

Kwa muda mrefu nchi ya Ethiopia imekuwa uwanja wa mapigano kati ya vikosi vya jeshi la serikali na kundi la waasi la Tigray People's Liberation Front (TPLF). Mapigano kati ya vikosi vya serikali na kundi la TPLF yalianza Novemba 4, 2020, wakati maafisa wa eneo la Tigray walipofanya uchaguzi wa serikali za mitaa kinyume na matakwa ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed. Waziri Mkuu wa Ethiopia anasema serikali ya Tigray si halali na kwamba inafanya jitihada za kulidhibiti eneo hilo kwa kutumia mabavu. Hali hii imeifanya serikali kuu kuanzisha vita dhidi ya wapiganaji wa kundi la TPLF. Lakini vita hivi vimepanuka zaidi katika maeneo mbalimbali ya Ethiopia katika miezi ya hivi karibuni. Vita hivyo vilivyosababisha vifo vya mamia ya watu na kujeruhi wengine wengi hatimaye vilisitishwa mwezi uliopita baada ya wapiganaji wa kundi la Tigray People's Liberation Front kurudi nyuma. Harakati hiyo imesema imeamua kurudi nyuma ili kuonyesha nia njema katika jitihada za kukomesha mgogoro wa nchi hiyo. 

Waasi wa TPLF  

Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, amewasamehe baadhi ya wafungwa wa kisiasa na kutangaza kukaribia kuanza kwa mazungumzo ya kitaifa ili kumaliza mgogoro huo. Taarifa iliyotolewa na serikali ya Ethiopia imesema madhumuni ya msamaha huo ni kuandaa njia ya kupatikana suluhu ya kudumu ya matatizo ya Ethiopia na kuongeza kuwa: "Ufunguo wa kuwepo umoja endelevu ni mazungumzo, na Ethiopia itafanya kila liwezekanalo kwa ajili ya suala hilo." 

Japokuwa hatua hiyo ya Abiy Ahmed imepongezwa na taasisi za ndani na za kimataifa, lakini shambulio la ghafla la Jeshi la Ethiopia katika kambi ya wakimbizi kaskazini mwa nchi hiyo lililosababisha vifo vya watu 56 na kujeruhi wengine wengi, kwa mara nyingine tena limeiweka nchi hiyo katika hatari ya kutumbukia vitani. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Henrietta Fore, ameeleza kukerwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya anga dhidi ya kambi za wakimbizi katika eneo la Tigray huko Ethiopia, akisema mashambulizi katika eneo hilo yamesababisha vifo vya makumi ya raia wakiwemo watoto wengi na kujeruhi wengine wengi.

Katika kipindi hiki ambapo Ethiopia inasumbuliwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na ukame, matatizo ya mpaka na majirani zake, mivutano iliyosababishwa na ujenzi wa Bwawa la Renaissance na umaskini na uhaba wa chakula unowakabili wakazi wengi wa mikoa ya kaskazini mwa nchi hiyo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema zaidi ya watu 400,000 huko Tigray wanaishi katika njaa.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths pia hivi karibuni aliutaja mgogoro wa eneo la Tigray nchini Ethiopia kuwa ni doa la aibu kwa walimwengu.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu, Martin Griffiths

Mzozo unaoendelea kati ya serikali ya serikali ya Ethiopia na kundi la waasi wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray kwa ajili ya kuliondoa madarakani kundi hilo umeweka hatarini umoja dhaifu wa Ethiopia na kutishia amani ya eneo la Pembe ya Afrika.

Katika hali hii, inaonekana kwamba kufanya mazungumzo ya kitaifa na kutatua mizozo wa Tigray  kunaweza kuzuia maafa zaidi ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Ethiopia.

Tags