Mar 10, 2022 14:33 UTC
  • Ripoti ya Mkaguzi Mkuu: 47% ya Wafanyikazi wa Hospitali ya Rufaa ya Kenyatta wanatoka kabila moja

Ripoti mpya inaonyesha kuwa kabila moja linaunda karibu nusu ya wafanyikazi wa Hospitali ya Rufaa na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Kenyatta (KUTRRH nchini Kenya.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Nancy Gathungu, imebainisha kuwa 285 kati ya wafanyakazi 608 wa Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, wanatoka katika jamii ya kabila moja. Amesema hii inawakilisha asilimia 47 ya jumla ya wafanyakazi wa hospitali hiyo.

Kwa mujibu wa matokeo ya ripoti ya Gathungu, suala hilo ni ukiukaji wa kifungu cha 7(1) na (2) cha Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa ya 2008.

Sheria hiyo inakataza jamii moja kumiliki zaidi ya thuluthi moja ya nafasi za ajira katika makampuni yanayomilikiwa na serikali.

Katika utetezi wao, wasimamizi wa hospitali hiyo wamesema ukosefu wa usawa katika ajira umesababishwa na ugonjwa wa COVID-19.

Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta umesema ukosefu wa usawa katika ajira umesababishwa na kuajiriwa watu kwa haraka wakati kituo hicho cha afya kilipotangazwa kuwa kituo cha kitaifa cha matibabu na wagonjwa wa COVID-19.

Iwapo Bunge la Kenya litachukua hatua kuhusu ripoti hiyo, wabunge wanaweza kuilazimisha Hospitali ya Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kutoa nafasi kwa makabila mengine.

Bunge la Kenya

Katika habari nyingine, Wakikuyu na Wakalenjin wanaongoza orodha ya jamii zilizo na uwakilishi mkubwa katika utumishi wa umma nchini Kenya. Hii ni wka mujibu wa ripoti iliyotolewa Disemba mwaka 2020.

Vilevile ukaguzi wa ajira ulionyesha kuwa jamii za Waluhya, Mijikenda na Turkana zilikuwa na uwakilishi mdogo katika utumishi wa umma.

Tags