Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia anusurika kuuawa na magaidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81838-waziri_wa_mambo_ya_ndani_wa_tunisia_anusurika_kuuawa_na_magaidi
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia, Taoufik Charfeddine amenusurika kuuawa katika shambulio linaloaminika kuwa la kigaidi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 27, 2022 08:00 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia anusurika kuuawa na magaidi

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tunisia, Taoufik Charfeddine amenusurika kuuawa katika shambulio linaloaminika kuwa la kigaidi.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Tunis hapo jana, Msemaji wa Gadi ya Taifa, Houcemeddine Jbabli amesema waziri huyo nusura auawe kwa kuchomwa kisu alipoutembelea mji wa Douz, ulioko katika mkoa wa Kebili, Kusini Mashariki mwa nchi.

Amesema maafisa usalama walizima na kusambaratisha mtandao mmoja wa kigaidi uliokuwa umepanga kumvizia na kumuua Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo, Taoufik Charfeddine kwa kumpiga jambia.

Jbabli amesema Idara ya Kupambana na Ugaidi katika Gadi ya Taifa ya nchi hiyo imefanikiwa kuwatia mbaroni magaidi 55 wakufurishaji pamoja na viongozi wao tokea mwanzoni mwa mwezi huu, na kwamba katika kipindi cha miezi sita iliyopita wamefanikuwa kuvunja mitandao 148 ya kigaidi.

Kuna hofu ya kuchipuka tena magenge ya kigaidi Tunisia

Haya yanajiri siku chache baada ya askari usalama nchini Tunisia kufanikiwa kusambaratisha mtandao mmoja wa kigaidi ujulikanao kwa jila la "al Muwahhidun" katika miji wa Tataouine na Soussa ya Kusini mwa mji mkuu, Tunis.

Tunisia imeamua kuchukua hatua zaidi za tahadhari baada ya kuongezeka wasiwasi wa kurejea tena magenge ya kigaidi na ukufurishaji huko Kaskazini mwa Afrika.