Jun 05, 2022 02:39 UTC
  • Morocco yaonywa kuhusu hatari ya kujipenyeza utawala wa Kizayuni nchini mwao

Taasisi ya Kupiga Vita Uhusiano wa Kawaida na Israel ya nchini Morcco imeionya serikali ya nchi hiyo kuhusu hatari ya kuruhusu utawala wa Kizayuni kuwa na ushawishi nchini humo.

Mwaka 2020, Morocco iliingia kwenye mkumbo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mashinikizo makubwa ya Marekani na kudharau jinai zote zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu mkuu wa taasisi hiyo ya Morocco akilaani kutiwa saini hati ya maelewano baina ya Wizara ya Elimu ya nchi hiyo na ile ya utawala wa Kizayuni kwa ajili ya kushirikiano kisayansi na kiteknolojia na kuwataka wananchi wa Morocco kuwa macho mbele ya hatari ya kuenea ushawishi wa utawala wa Kizayuni nchini mwao.

Mfalme wa Morocco, Mohamed VI

 

Amesema, msimamo wa Wizara ya Elimu ya Morocco ambayo imejitumbukiza kwenye mkumbo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, ni jambo la hatari sana ambalo lina madhara makubwa kwa jamii wa Morocco. 

Pia amesema, Wamorocco wanapaswa kuwa macho mbele ya hatari za Wazayuni hao na kwamba kujidhalilisha kwa Wazayuni ni ishara ya kuanza hesabu ya kinyumenyume ya kupromoka utawala wa kifalme wa Morocco.

Mwanaharakati huyo wa kisiasa wa Morocco amesisitiza kuwa, kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya Wizara za Elimu za Morocco na utawala wa Kizayuni ni mwanzo tu wa kuzidi kujipenyeza utawala wa Kizayuni ndani ya jamii wa Wamorocco.

Amesema, iwapo jambo hilo litaendelea, bila ya shaka wananchi wa Morocco watakula hasara kubwa na wakati huo hawatobakiwa na chochote zaidi ya kujuta na kutamani siku zirudi wasimame imara kuzuia kujipenyeza Wazayuni nchini mwao.

Tags