Aug 26, 2022 07:05 UTC
  • Mgogoro wa nishati Ufaransa wamlazimisha Macron kuzuru koloni la zamani

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amewasili Algeria, koloni la kitambo la nchi hiyo ya Ulaya katika safari inayolenga kuitaka nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika iongeze kiwango cha gesi inayouza barani Ulaya.

Katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Rais Abdelmajid Tebboune wa Algeria jijini Algiers hapo jana, Macron alidai kuwa, "Tunataka kufungua ukurasa mpya wa uhusiano wa pande mbili, hatukuchagua jadi yetu, bali tulirithi."

Weledi wa mambo wanasema safari ya Macron nchini Algeria imechochewa na mgogoro wa nishati unaoikumba Ufaransa pamoja na nchi nyingine za Ulaya. Mauzo ya gesi ya Russia kwa Ulaya yamepungua sana na kuziacha nchi nyingi za bara hilo zikikumbwa na tatizo la kujidhaminia nishati na kuongezeka gharama ya bidhaa hiyo muhimu.

Serikali ya Algeria Oktoba mwaka jana ilimwita nyumbani kwa mashauriano balozi wake mjini Paris kufuatia matamshi dhidi ya Algeria ya Rais Emmanuel Macron. Rais wa Ufaransa aliwahi kudai kuwa historia ya Algeria haitokani na uhakika wa mambo bali matamshi ya chuki dhidi ya Ufaransa.

Tebboune amenukuliwa mara kadhaa huko nyuma akisisitiza kuwa,  wananchi wa Algeria hawatasahau jinai na uhalifu uliofanywa na Ufaransa katika enzi za ukoloni, na kwamba mkoloni Mfaransa hajailetea Algeria manufaa yoyote ghairi ya kuisababishia nchi hiyo uharibifu na maafa.

Alisema, faili la jinai za Wafaransa nchini Algeria linapasa kuchunguzwa kwa haki na uwazi, na kwamba ukoloni wa Ufaransa nchini kwake kuanzia mwaka 1830 hadi 1962 ulifanya uhalifu wa kutisha sana ambao haujashuhudiwa katika historia ya sasa ya mwanaadamu. Zaidi ya Waalgeria milioni moja waliuliwa na wanajeshi wa Ufaransa katika kipindi cha vita vya kupigania ukombozi wa Algeria kuanzia mwaka 1954 hadi 1962.  

Tags