Mpango wa UK wawaacha bila makazi wahanga wa mauaji ya kimbari Rwanda
Wahanga wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda waliofurushwa katika mabweni walikokuwa wakiishi kutokana na mpango tata wa wakimbizi wa Uingereza, wanalalamika kuwa wameachwa bila pahala pa kuishi, licha ya mabweni hayo kusalia bila watu.
Wahanga hao wa mauaji ya kimbari ya Rwanda yaliyopelekea watu zadi ya laki 8 kuuawa mwaka 1994, na ambao wamekuwa wakiishia katika Bweni la Hope jijini Kigali kwa zaidi ya miaka 8, waliamrishwa kuondoka kwenye jengo hilo, ili kupisha wakimbizi wanaotazamiwa kupelekwa nchini humo kutoka Uingereza.
Wahanga hao wapatao 190 walifurushwa kwenye mabweni hayo siku mbili baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, Priti Patel kusaini makubaliano hayo ya kutatanisha na serikali ya Rwanda, ya pauni milion 120.
Mpango huo wa Uingereza wa kuwapeleka wakimbizi Rwanda kwa nguvu bila hiari yao umekosolewa vikali na duru mbalimbali za ndani na nje ya Rwanda na Uingereza kwenyewe.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR Filippo Grandi, amekosoa vikali uamuzi wa serikali ya Uingereza wa kuwahamishia Rwanda watafuta hifadhi wanaokwenda nchini humo huku akisema makubaliano hayo ya kando kati ya nchi mbili hizo ni makosa.sawa na kufunguliwa ukurasa wa giza katika haki za kimataifa za wakimbizi.
Alisisitiza kuwa, Rwanda ilikuwa na historia ya kipekee ya kukaribisha na kusaidia maelfu ya wakimbizi kutoka DRC na Burundi, na akaongezea kwa kusema, nchi hiyo haina uwezo na miundombinu ya kuhudumia wakimbizi kwa kuzingatia mahitaji ya sasa.