Wanajeshi wa Libya waukomboa kikamilifu mji wa Sirte
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i8938-wanajeshi_wa_libya_waukomboa_kikamilifu_mji_wa_sirte
Vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya vimetangaza habari ya kuukomboa kikamilifu mji wa kistratajia wa Sirte, uliokua chini ya udhibiti wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 11, 2016 02:41 UTC
  • Wanajeshi wa Libya waukomboa kikamilifu mji wa Sirte

Vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya vimetangaza habari ya kuukomboa kikamilifu mji wa kistratajia wa Sirte, uliokua chini ya udhibiti wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.

Taarifa ya jeshi la Libya imesema kuwa, kufuatia makabiliano makali kati ya vikosi hivyo vya serikali na kundi la Daesh jana Ijumaa, sasa mji huo bandari uko chini ya udhibiti wao kikamilifu. Hapo jana, duru za habari ziliripoti habari ya kukombolewa kikamilifu fukwe za mji wa Sirte na maeneo mengine muhimu ya mji huo ambao kundi la Daesh lilikuwa limeufanya kuwa ngome yake. Taarifa zinasema kuwa, maeneo kadhaa muhimu katika viunga vya mji wa Sirte kama vile uwanja mmoja wa ndege, vituo kadhaa vya kijeshi na barabara moja kuu yamekombolewa kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh. Habari zaidi zinasema kuwa, vikosi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya vingali vinaendeleza operesheni katika kila kona ya mji huo ili kuusafisisha kabisa na kuhakikisha kuwa hauna hata mwanachama mmoja wa Daesh. Shirika la habari la Reuters limemnukuu kamanda mmoja wa vikosi hivyo aliyesema kuwa, kwa akali askari 11 wa serikali wameuawa katika operesheni ya kuukomboa mji huo muhimu wa bandari. Libya ilitumbukia katika wimbi la machafuko baada ya kuondolewa madarakani utawala wa Kanali Muammar Gaddaf, mtawala wa zamani wa nchi hiyo. Machafuko hayo yalitoa mwanya kwa makundi ya kigaidi hususan Daesh kuweza kujipenyeza nchini humo na kudhibiti miji.