Mali yawahukumu wanajeshi wa Ivory Coast miaka 20 jela
(last modified Sun, 01 Jan 2023 07:34:42 GMT )
Jan 01, 2023 07:34 UTC
  • Mali yawahukumu wanajeshi wa Ivory Coast miaka 20 jela

Mahakama moja huko Bamako, mji mkuu wa Mali imewahukumu kifungo cha miaka 20 jela makumi ya wanajeshi wa Ivory Coast baada ya kuwapata na hatia ya 'kuhujumu' usalama wa taifa hilo jirani yake.

Hukumu ya Mahakama ya Rufaa ya Bamako imetolewa siku mbili tu baada ya kuanza mchakato wa kasi wa kusikilizwa kwa kesi dhidi ya wanajeshi hao wa Kodivaa Alkhamisi ya Disemba 29.

Wadadisi wa mambo wameonya kuwa, hukumu hiyo na matukio yanayoendelea hivi sasa kati ya Ivory Coast na Mali yanaweza kuathiri amani na utulivu wa eneo zima la Magharibi mwa Afrika.  

Mali na Ivory Coast zilitumbukia katika mzozo wa kidiplomasia tangu Julai 10 mwaka uliomalizika 2022, baada ya maafisa wa Mali kuwatia nguvuni wanajeshi 46 wa Ivory Coast mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bamako.

Serikali ya Mali inayoongozwa na wanajeshi ilisema kuwa, wanajeshi hao wa Ivory Coast hawakuwa na nyaraka zozote za kuarifisha ujio wao huko Mali na kwamba iliwatambua kama mamluki. Wanajeshi hao walituhumiwa kujaribu kuvuruga usalama wa Mali na kisha wakaweka korokoroni. 

Wanajeshi wa Kodivaa

Serikali ya Ivory Coast kwa upande wake ilisema kuwa wanajeshi hao walikwenda Mali kwa ajili ya shughuli za kawaida za kuunga mkono kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Mali.

Ivory Coast hapo awali iliishutumu Mali kwa kuidai fidia na kuamiliana na wanajeshi wake hao 46 kama wahalifu baada ya kutiwa nguvuni na serikali ya Bamako. Serikali ya Ivory Coast imewaomba mara kadhaa viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS kujadili hali hiyo ya mgogoro kati yake na Bamako haraka iwezekanavyo.