Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu waripotiwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9808-ukiukaji_mkubwa_wa_haki_za_binadamu_waripotiwa_kongo
Umoja wa Mataifa umesema kuwa una wasiwasi na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2016 11:23 UTC
  • Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu waripotiwa Kongo

Umoja wa Mataifa umesema kuwa una wasiwasi na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema katika ripoti yake ya kila mwezi iliyotolewa jana kuwa vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu ambavyo vyanzo vyake ni masuala ya kisiasa vimejiri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vitendo 371 vya ukiukaji wa haki za binadamu vimeripotiwa nchini Kongo katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka huu wa 2016; ambapo mwaka jana 2015 kuliripotiwa vitendo 260 vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini humo. Umoja wa Mataifa umesema katika ripoti yake hiyo kuwa, mwezi Mei mwaka huu ni mwezi mbaya zaidi kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu kwa sababu, jumla ya vitendo 155 vya ukiukaji wa haki za binadamu vimesajiliwa katika mwezi huu pekee huko Kongo. Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, mrengo wa upinzani nchini Kongo uliitisha maandamano karibu mara 300 katika mwezi wa Mei mwaka huu; maandamano ambayo hata hivyo yalipigwa marufuku au kukandamizwa na vikosi vya usalama na polisi wa nchi hiyo. Ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imeeleza kuwa ghasia na machafuko hayasababishwi na makundi yenye silaha huko Kongo bali ni natija ya hatua za polisi wa nchi hiyo ambazo ni mfano wa wazi wa ukiukaji wa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza nchini humo.