Jun 24, 2016 14:44 UTC
  • Rufaa ya Zuma kupinga kufufuliwa kesi za ufisadi dhidi yake yakataliwa

Mahakama Kuu mjini Pretoria nchini Afrika Kusini imetupilia mbali rufaa ya Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ya kupinga kufufuliwa kesi za ufisadi wa kifedha dhidi yake, hatua ambayo ni pigo kwa rais huyo ambaye anakabiliwa na mashinikizo ya kujiuzulu kutoka viongozi wa upinzani.

Katika uamuzi huo wa leo Ijumaa, Jaji Aubrey Ledwaba wa mahakama hiyo amesema ingawa rufaa hiyo ni muhimu kwa Rais Zuma, lakini imetupilia mbali kwa kuwa haina msingi. Rais Zuma pamoja na Shaun Abrahams, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma nchini humo waliitaka mahakama hiyo ikubali rufaa hiyo iliyowasilishwa mapema mwezi huu. Itakumbukwa kuwa, tarehe 10 mwezi huu, Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini alikata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuagiza kufufuliwa kesi zaidi ya 700 za ufisadi wa kifedha dhidi yake. Ofisi ya Zuma ilisema kuwa, Mahakama Kuu ilikosea kutoa uamuzi wa kufufuliwa kesi 783 za ufisadi dhidi ya rais huyo, licha ya kuwa zilikuwa zimebatilishwa huko nyuma na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma. Mwishoni mwa mwezi wa Aprili mwaka huu, Mahakama Kuu ya mjini Pretoria ilisema kuwa, uamuzi uliotolewa mwaka 2009 wa kutupilia mbali kesi zilizohusu madai ya ufisadi dhidi ya Rais Zuma, haukuwa na mantiki na kwa msingi huo, kesi hizo zinafaa kusikilizwa upya. Vyama vya upinzani nchini humo kikwemo cha Economic Freedom Fighters chake Julius Malema, kinara wa upinzani katika nchi hiyo ya kusini mwa Afrika vinashikilia kuwa, uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ni sahihi na kesi hizo dhidi ya Zuma zinafaa kusikilizwa upya. Tuhuma hizo zinahusiana na manunuzi ya silaha yenye gharama za mabilioni ya dola hapo mwaka 1999 ambapo kwa mujibu wake, kipindi hicho Afrika Kusini ilitumia mabilioni ya dola kununua silaha za kivita kutoka shirika moja la silaha la nchini Ufaransa.

Tags