Wakati Israel ilipofedheheshwa katika mkutano wa IPU; Tulia Ackson ajitetea kwa nguvu zote + Video
(last modified 2024-10-16T11:02:14+00:00 )
Oct 16, 2024 11:02 UTC

Wabunge wa nchi mbalimbali duniani wameususia utawala wa Kizayuni wa Israel na kutoka nje ya ukumbi wakipiga nara za ukombozi wa Palestina wakati wa Mkutano Mkuu wa 149 wa Muungano wa Mabunge ya Umoja wa Mataifa (IPU) mjini Geneva, Uswisi.

Kikao hicho kilichoongozwa na Rais wa IPU, Tulia Ackson kimeshuhudia fedheha nyingine ikiukumba utawala wa Kizayuni baada ya wajumbe kutoka kwenye ukumbi huku sauti ya "Free Free Palestine" ikifunika anga yote ya ukumbi huo.

Wawakilishi kutoka nchi nyingi waligonga meza zao kutangaza kukasirishwa kwao na jinai za Israel na kisha wametoka nje ya ukumbi.

Wabunge hao walirejea ukumbini baada ya hotuba ya afisa huyo wa Israel kumaliza kutoa hotuba yake na kuendelea na kikao.

Spika wa Bunge la Tanzania, Tulia Ackson

 

Amma kwa upande wake, Rais wa Muungano wa Mabunge ya Umoja wa Mataifa (IPU)  Tulia Ackson ambaye pia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametetea utendaji wa IPU katika kutatua migogoro ukiwemo wa hivi sasa katika eneo la Asia Magharibi.

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kufanya jinai kubwa dhidi ya Palestina na Lebanon huku idadi ya wananchi wa Lebanon waliouliwa kikatili na Israel tangu Septemba 23 wakipindukia 1,500 na zaidi ya milioni moja kuyahama makazi yao.

Kwa huko Ghaza, utawala wa Kizayuni umeshaua kikatili Wapalestina 42,400, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo tangu Oktoba 7, 2023.