Aug 08, 2023 03:09 UTC
  • Iran yakosoa tuhuma zisizo na maana za Uingereza dhidi ya IRGC

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali madai yasiyo na msingi ya Uingereza dhidi Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC).

Katika kikao na waandishi wa habari hapa mjini Tehran jana Jumatatu, Nasser Kan'ani amelaani tuhuma bandia za Uingereza dhidi ya IRGC na kusisitiza kuwa, jeshi hilo la Iran limepambana na magaidi waliofadhiliwa na Wamagharibi katika eneo la Asia Magharibi.

Ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya Suella Braverman, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza dhidi ya SEPAH na kueleza kuwa, "Uingereza haina ustahiki wa kimaadili wa kuibua tuhuma za namna hii dhidi ya IRGC ambayo imekabiliana na ugaidi uliofadhiliwa na UK kwa miongo kadhaa."

Kan'ani amebainisha kuwa, Uingereza ina historia nyeusi Asia Magharibi, kwa kuwa mbali na kusababisha ukosefu wa uthabiti katika eneo, lakini pia imekuwa ikiunga mkono harakati za kigaidi kwa siri na kwa dhahiri katika eneo.

Wanajeshi wa IRGC

Kauli ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ni jibu kwa bwabwaja za hivi karibuni za Suella Braverman, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza aliyedai kuwa IRGC ndilo tishio kuu la usalama kwa UK hivi sasa.

Kwa mujibu wa Kan'ani, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran si tu limetoa huduma nyingi kwa nchi za eneo la Mashariki ya Kati, bali pia kwa mataifa ya Ulaya.

 

Tags