Aug 19, 2023 11:25 UTC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kupanga na kufadhili mapinduzi, kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kuwaunga mkono madikteta ni katika sera kuu za Marekani na Uingereza katika kipindi chote cha historia.

Nasser Kan'ani amesema hayo katika ujumbe aliotuma leo kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X (Twitter) na kueleza kuwa: Miaka 70 iliyopita, serikali ya kitaifa nchini Iran iliondolewa madarakani katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani na Uingereza.

Amebanisha kuwa, sera za nje za Marekani na Uingereza zimejengeka katika misingi ya kuwaunga mkono na kuwakingia kifua madikteta, kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine, na kupanga mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali halali katika pembe mbalimbali za dunia.

Kan'ani amesema hayo kwa mnasaba wa kutimia miaka 70, tangu yatokee mapinduzi ya kijeshi ya Agosti 19, 1953 (Mordad 28, 1332), ambayo yalipelekea kupinduliwa serikali ya Waziri Mkuu wa Iran wakati huo Mohammad Mosaddegh.

Serikali ya Uingereza ilikuwa ndiye mpangaji mkuu wa mapinduzi hayo ya Mordad 28, na Marekani ilitoa mchango muhimu na athirifu katika kufanikisha mpango huo.

Kuuzuliwa kwa Mosaddegh kulikofanyika miaka 70 iliyopita yalikuwa matokeo ya njama na hatua za pamoja zilizochukuliwa na mashirika ya kijasusi ya CIA ya US na MI6 ya UK

Baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, Washington, ikishirikiana bega kwa bega na London, ilianza hatua kwa hatua kuingilia masuala ya ndani ya Iran; na katika kufanikisha mpango huo, ilishirikiana na Uingereza na kujihusisha moja kwa moja katika kupanga na kutekeleza mapinduzi ya Agosti 1953, dhidi ya serikali ya kitaifa ya Waziri Mkuu Mohammad Mossadegh.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa, ni hulka na dhati ya Marekani na Uingereza kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na kupanga mapinduzi, muda wote zinapotaka kupigania maslahi yao.

Tags