Spika: Uanachama wa Iran katika BRICS una manufaa ya kisiasa na kiuchumi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i102714-spika_uanachama_wa_iran_katika_brics_una_manufaa_ya_kisiasa_na_kiuchumi
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kupewa uanachama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kundi la BRICS kuna umuhimu mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na hata kijiografia.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Sep 26, 2023 10:22 UTC
  • Spika: Uanachama wa Iran katika BRICS una manufaa ya kisiasa na kiuchumi

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kupewa uanachama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kundi la BRICS kuna umuhimu mkubwa wa kisiasa, kiuchumi na hata kijiografia.

Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran amesema hayo leo Jumanne kabla ya kuondoka hapa nchini kuelekea Afrika Kusini, anakoenda kushiriki mkutano wa Jukwaa la Tisa la Mabunge ya BRICS.

Ameeleza bayana kuwa, "Nchi tatu kati ya tano kuu wanachama wa BRICS zina umuhimu mkubwa kijiografia." Qalibaf ameongeza kuwa, kupewa uanachama Iran katika kundi la BRICS kumesambaratisha sera ya Marekani ya kujaribu kuitenga Jamhuri ya Kiislamu.

Mkutano wa Jukwaa la Tisa la Mabunge ya BRICS pamoja na mambo mengine, unatazamiwa kujadili sera ya kambi kadhaa, na uimarishwaji wa uhusiano baina ya nchi za Afrika na wanachama wa kundi la BRICS.

Spika wa Bunge la Iran amebainisha kuwa, kukubaliwa Iran kuwa mwanachama wa BRICS kumethibitisha kujitolea kwa nchi hii kuimarisha ushirikiano na nchi za dunia, na kufanikiwa kwake kuvunja mradi wa Marekani wa kulitenga taifa hili.

Iran pamoja na nchi nyingine tano zilikubaliwa kujiunga na kundi la BRICS katika mkutano wa 15 wa kilele wa jumuiya hiyo ya kiuchumi uliofanyika hivi karibuni huko Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Kadhalika Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema anatumai safari yake ya Afrika Kusini itakuwa na mchango athirifu katika kuimarisha uhusiano wa kibunge wa Iran na nchi wanachama wa BRICS, ikiwemo Afrika Kusini.