Shahriari: Uhusiano wa Iran na Saudia unaimarisha umma wa Kiislamu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu amesema kurejeshwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia kumesaidia kuboreka umoja na matumaini katika ulimwengu wa Kiislamu.
Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, Hujjatul Islam Hamid Shahriari, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu alisema hayo jana Jumapili katika ufunguzi wa Kongamano la 37 la Kimataifa la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran na kuongeza kuwa, kuwepo uhusiano wa karibu kati ya Iran na Saudia ni hatua nzuri kwa ajili ya kuimarisha usalama, utulivu na amani katika eneo.
Amesema, "Ushirikiano na urafiki miongoni mwa nchi za Kiislamu unatia nuru kwenye nyoyo za wanaopigania mwamko katika umma wa Kiislamu."
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Pamoja Madhehebu za Kiislamu sanjari na kuzipongeza serikali za Tehran na Riyadh kwa kuhuisha uhusiano wa pande mbili ameeleza bayana kuwa, nchi za Kiislamu zinaweza kuelekea kwenye umma mmoja madhubuti kwa kushirikiana.
Hujjatul Islam Shahriari amebainisha kuwa, kuimarika uhusiano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudia pamoja na nchi za eneo la Asia Magharibi kutanufaisha ulimwengu wa Kiislamu.
Kiwango cha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili za Kiislamu za Iran na Saudi Arabia ni cha hali ya juu hivi sasa, na viongozi wa nchi zote hizi mbili wamesisitiza juu ya nia yao wa kuimarisha zaidi ushirikiano wao katika nyuga nyinginezo hasa za kiuchumi.
Nchi mbili za Iran na Saudia zilirejesha uhusiano wao tarehe 10 Machi 2023 kwa upatanishi wa China, baada ya kupita miaka 7 ya Saudia kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran.