Amir Abdollahian: Hali ya Syria imekuwa ngumu kutokana na uingiliaji wa Marekani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika kikao na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Syria kwamba hali ya Syria imekuwa ngumu kutokana na uingiliaji wa Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza katika kikao hicho ulazima wa kuiunga mkono serikali ya Syria katika kuendeleza mapambano dhidi ya ugaidi na kusema: Hali ya Syria imekuwa ngumu kutokana na uingiliaji wa Marekani na ushawishi wake kwa makumi ya makundi ya kigaidi ambayo yanaendelea kutishia usalama wa nchi hiyo.
Amir Abdullahian amevitaja vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Syria kuwa ni hatua dhidi ya taifa la Syria na kumtaka mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu na Naibu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu kufanya juhudi kwa ajili ya kuondolewa vikwazo hivyo.
Katika kikao hicho naye Mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea juhudi na mipango yake ya kusaidia kuutatua mgogoro wa Syria na kueleza matumaini yake kuwa, matukio ya sasa ya Palestina hayatakuwa na taathira hasi kwa hali ya Syria.
Kikao cha Waziri wa Mambo ya Nje na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria kilikuwa cha mwisho kufanyika katika safari yake huko Geneva.
Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje alikuwa na vikao kadhaa na viongozi wa Umoja wa Mataifa, akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu, Mabalozi na Wawakilishi wa mashirika ya kimataifa yanayohusika na haki za binadamu, ambapo vyote vilihusu kuwasaidia watu wanaodhulumiwa wa Gaza na kuzuia mauaji ya kikatili ya Wapalestina yanayofanywa na Wazayuni.