Iran: US ndiyo sababu ya kushtadi mgogoro Ukanda wa Gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haitaki vita vya Gaza vipanuke, lakini yumkini vitasambaa zaidi katika maeneo mengine kwa kuwa Marekani inachochea mgogoro huo kwa kuuunga mkono utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hossein Amir-Abdollahian ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya CBS na kuongeza kuwa, kuna haja ya kufanyika jitihada za kukomesha mashambulizi ya Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hasa wanawake na watoto wadogo.
Amesema Marekani inabeba dhima ya kuendelea uvamizi na hujuma za kinyama dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kwamba jamii ya kimataifa ina wajibu wa kusimamisha vita hivyo mara moja.
Kadhalika Amir-Abdollahian amesema hatua ya utawala wa Kizayuni kulenga shule, hospitali, ambulensi na vituo vya kutoa huduma za afya katika mashambulizi yake ya kikatili huko Ukanda wa Gaza ni jinai za kivita.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya harakati ya kupigania ukombozi wa Palestina Hamas kufanya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel, ikiwa ni jibu kwa jinai za miongo kadhaa za utawala huo katili dhidi ya Wapalestina.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, hadi sasa Israel imewaua shahidi Wapalestina 11,500, wakiwemo watoto 4,630 na wanawake 3,130, na kujeruhi wengine zaidi ya 32,000.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa: Kwa hakika, hatutaki mgogoro huu (wa Gaza) upanuke, lakini Marekani kwa kuiunga mkono Israel imeshadidisha hali ya mambo. Iwapo jinai dhidi ya watu wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan zitaendelea, hakuna shaka mgogoro huo utaenea (katika maeneo mengine ya Asia Magharibi).