Nov 19, 2023 13:21 UTC
  • Iran yazindua kombora la hypersonic la 'Fattah 2'

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua kombora jipya la hypersonic lililopewa jina la 'Fattah 2'.

Kombora hilo la aina yake limezinduliwa leo Jumapili wakati Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei alipotembelea maonyesho ya mafanikio ya Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Maonyesho hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Anga za Mbali cha Ashura, ambapo Kikosi cha Anga za Mbali cha Jeshi la SEPAH limezindua silaha na zana mbalimbali za kijeshi likiwemo kombora la Fattah 2.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, kombora hilo lina kasi kubwa na uwezo wa aina yake, na hakuna teknolojia yoyote duniani inayoweza kulitungua hata katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo.

Kombora hilo la cruise lililozinduliwa kama bidhaa mpya kabisa ya makombora yaliyoundwa na sekta ya viwanda vya Wizara ya Ulinzi ya Iran, lipo katika safu ya makombora ya hypersonic yenye uwezo mkubwa ya HGV na HCM.

Kiongozi Muadhamu katika uzinduzi wa silaha mpya za Iran

Aidha katika maonyesho hayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua mfumo wa ulinzi wa 'Mehran', mfumo ulioimarishwa wa 'Dey 9' na ndege isiyo na rubani (droni) ya 'Shahed-147'.

Ikumbukwe kuwa, Juni mwaka huu 2023, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilizindua kombora lake la kwanza la balistiki la hypersonic lililopewa jina la 'Fattah'.

Kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani, Waziri wa Ulinzi wa Iran, sekta ya viwanda vya Wizara ya Ulinzi ya Iran ina uwezo wa kuunda silaha za aina zozote zinazohitajika na vikosi vya ulinzi vya nchi hii.

Mafanikio ya viwanda vya silaha vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika kuunda makombora ya balistiki katika miaka ya karibuni yameyatia tumbojoto madola ya Magharibi. 

Tags