Dec 26, 2023 08:58 UTC
  • Radiamali mbalimbali za kuuawa shahidi mshauri wa kijeshi wa Iran nchini Syria

Kamanda Sayyid Razi Mousavi, mmoja wa washauri wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH), ambaye alikuwa akifanya kazi katika uga wa utoaji misaada ya kilojistiki kwa Mhimili wa Muqawama wa Syria, aliuawa shahidi katika shambulio lililofanywa jana Jumatatu na utawala wa Kizayuni katika eneo la Zainabiyah mjini Damascus.

Kamanda huyo mwandamizi na mashuhuri wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alishanusurika mara kadhaa katika majaribio ya kumuuua shahidi yaliyowahi kufanywa na jeshi la kigaidi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.

Kamanda Mousavi maarufuku kwa jina la Sayyid Razi, ni mmoja wa washauri wakongwe wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na mmoja wa wapiganaji wa kipindi cha kujihami kutakatifu. Alikuwa kamanda shupavu ambaye alishiriki katika operesheni nyingi za kijeshi bega kwa bega na wapiganaji wa Iran wakati wa vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na dikteta wa wakati huo wa Iraq Saddam dhidi ya taifa hili. Aidha alikuwa mmoja wa masahiba wa kamanda mkuu wa Iran wa kupambana na ugaidi, shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani.

Kufuatia kuuawa shahidi Kamanda Mouusavi, wakuu wa Mihimili Mikuu Mitatu ya Dola yaani Serikali, Bunge na Idara ya Mahakama nchini Iran wametoa risala na jumbe kwa nyakati tofauti ambapo sambaamba na kulaani mauaji hayo ya utawala ghasibu wa Israel huko Syria, wametoa mkono wa pole kwa kuuawa shahidi kamanda huyu wa Uislamu.

Katika ujumbe wake, Rais wa Iran, Ebrahim Raisi, amesema utawala wa Kizayuni wa Israel utalipa gharama ya kitendo chake cha uhalifu cha kumuua mshauri mkuu wa kijeshi wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) nchini Syria.

Rais wa Iran, Ebrahim Raisi

 

Aidha Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika sehemu nyingine ya ujumbe wake huo kwamba, kitendo kiovu cha kumuua kigaidi mshauri wa jeshi la SEPAH katika shambulio la makombora nchini Syria ni ishara nyingine ya kukata tamaa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Gholam-Hossein Mohseni-Ejei, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran naye ametoa ujumbe wa tanzia kwa mnasaba wa kuuawa shahidi Kamanda Sayyid Razi Mousavi na kulaani vikali jinai hiyo.

Kwa upande wake, Muhammad Bagher Qalibaf, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika ujumbe wake wa rambi rambi kwamba, hapana shaka kuwa, utawala mmwagaji damu wa Israel utalipa gharama ya jinai hii.

Wakati huo huo, kundi la wanachuo na wakazi wa mji wa Tehran jana usiku walikusaanyika mbele ya jengo la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa wa Iran na kutoa mwito wa kulipizwa kisasi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kwa damu ya shahidi Sayyid Razi Mousavi.

Sayyid Razi Mousavi (kushoto) akiwa na Kamanda Qassim Soleimani enzi za uhao wao

 

Katika mkusanyiko huo wa raia na wanachuo, ambao ulifanyika kufuatia mwito wa uhamasishaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Tehran, Amir Kabir na Allameh na uliopewa jina la "Wakati wa Jihadi", washiriki walibeba bendera ya Iran na harakati ya muqawama ya Hizbullah sambamba naamabango na maberamu yaliyokuwa na jumbe mbalimbali ambapo moja ya ujumbe huo ulisomeka:  "Hussein Hussein ni kaulimbiu yetu, kufa shahidi ni fakhari yetu."

Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza katika salamu za rambirambi za kuuawa shahidi Seyed Razi Mousavi, mmoja wa washauri wakuu wa kijeshi wa Iran nchini Syria kwamba, Tel Aviv inapaswa kusubiri siku ngumu.

Harakati ya Al-Nujaba ya Iraq pia imetoa taarifa na kusisitiza kuwa damu safi ya Brigedia Jenerali Seyyed Razi Mousavi, mmoja wa washauri wa SEPAH nchini Syria, kamwe haitapotea bure.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa viongozi wa utawala haramu wa Israel wana wasi wasi na hofu kubwa juu ya jibu ambalo Iran itatoa kwa mauaji ya Kamanda Sayyid Razi Mousavi, mshauri wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH).

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran

 

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRNA, gazeti la Kizayuni la Jerusalem Post, likiwanukuu maafisa wa utawala ghasibu wa Israel limeandika kuhusiana na suala hilo kuwa, Israel inatabiri kwamba Iran itajibu mapigo kwa kuuawa shahidi mshauri wa IRGC.

Kuhusiana na hilo, viongozi wa Kizayuni wamesema, jeshi la utawala huo linajiandaa kwa jibu ambalo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaweza ikatoa, ukiwemo uwezekano wa kufanya shambulio la makombora.

Jambo lisilo na shaka ni kama walivyosisitiza viongozi na maafisa mbalimbali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Rais Ebrahim Raisi ni kwamba, jinai hii ya utawala wa Kizayuni wa Israel haitapita hivi hivi bila ya majibu na hivyo Israel isuubiri kulipa gharama ya jinai yake hii.

Tags