Usalama kwenye uchaguzi; mafanikio muhimu ya kisiasa ya Iran
(last modified Wed, 28 Feb 2024 10:07:32 GMT )
Feb 28, 2024 10:07 UTC
  • Usalama kwenye uchaguzi; mafanikio muhimu ya kisiasa ya Iran

Moja ya mafanikio na matunda muhimu zaidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 45 iliyopita ni kufanyika chaguzi 39 katika mazingira salama na ya amani kamili.

Uchaguzi wa duru ya 12 ya Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu ya Iran na wa duru ya 6 wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran utafanyika Ijumaa, Machi 1 kote nchini. Moja ya masuala muhimu zaidi katika  uchaguzi ni kufanyika katika mazingira salama kabisa na yasiyokuwa na ghasia na mivutano.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa miito minne kuhusiana na uchaguzi wa Ijumaa, ambayo ni pamoja na kushiriki kwa wengi wananchi katika uchaguzi, kuwepo ushindani wa kweli, kuzingatiwa usalama na amani kamili wakati wa kufanyika uchaguzi. Kuhusiana na jambo hilo, Seyyed Majid Mir Ahmadi Naibu Afisa wa usalama katika Wizara ya Mambo ya Ndani na ambaye pia ni Mkuu wa Idara Kuu ya Usalama wa Uchaguzi nchini  alitangaza Jumatatu kuwa zaidi ya askari 250,000 wa jeshi, polisi na vyombo vya usalama watakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama unalindwa wakati wa uchaguzi.

Moja ya mambo yanayofanya usalama wa uchaguzi kupewa umuhimu mkubwa nchini Iran ni muundo wake wa makabila mengi. Iran ni nchi yenye makabila mengi na kushikiri kwa wengi kila kabila katika uchaguzi ni jambo muhimu mkubwa.

Pamoja na hayo, chaguzi 39 zilizopita nchini Iran, zilifanyika katika mazingira ya usalama kamili bila kushuhudiwa vurugu hata kidogo na jambo hilo linahesabiwa kuwa moja ya mafanikio ya wazi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uwanja huo.

Kiongozi Muadhamu akizungumza karibuni na vijana waliotimiza umri wa kupiga kura kwa mara ya kwanza

Kuhusiana na hilo, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: 'Sifa nyingine muhimu na ya kustaajabisha na kwa hakika tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo, ni uchaguzi kufanyika katika mazingira salama na ya amani licha ya kuwepo vichocheo vya kuibuka ghasia na mivutano. Kwa mfano uwepo wa makabila yanayofuatilia maslahi tofauti, miji miwili yenye maslahi kinzani na mashindano kati ya miji tofauti nchini ni masuala yanayoweza kuibua hitilafu na machafuko wakati wa kufanyika uchaguzi lakini pamoja na hayo hakuna tukio lolote uchungu lililoshuhudiwa katika uwanja huo.

Mbali na miji mikubwa nchini, hali hiyo ya utulivu wakati wa kufanyika uchaguzi imekuwa ikishuhudiwa katika miji, vijiji na pembe zote za nchi. Hakuna tukio lolote chungu ambalo limehatarisha usalama wa uchaguzi wala kupelekea maisha ya watu kupotea.

Mmojawapo wa sababu muhimu zinazomfanya kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu daima kusisitiza juu ya kufanyika uchaguzi katika mazingira salama ni kufikiwa malengo yaliyokusudiwa katika uchaguzi huo.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu anaamini kuwa uchaguzi nchini Iran unapaswa kuleta umoja. Alikumbusha kuhusiana na hilo, katika mkutano wa tarehe 18 February 2024, na watu wa Tabriz kuwa: 'tofauti za kibinafasi na kisiasa zisiathiri umoja wa kitaifa wa Iran katika kukabiliana na njama za  maadui.'

Mafanikio hayo muhimu na ya wazi yamepatikana katika hali ambayo maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa wakipanga na kutekeleza njama chungu nzima kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi kwa upande mmoja, na kuibua ghasia na machafuko kwa upande wa pili.

Kwa mujibu wa takwimu za vyombo vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, tangu mwezi Septemba uliopita, maadui wamekuwa wakifanya njama za kuibua ghasia na vurumai katika pembe tofauti za nchi kwa madhumuni ya kuzuia kufanyika uchaguzi Ijumaa Machi Mosi, njama ambazo zimeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa na hilo bila shaka linatokana na kuwa macho vyombo na taasisi za kiusalama nchini.