Ayatullah Khatami: Siku ya Quds itakuwa tofauti kabisa mwaka huu
Khatibu wa Swala ya Ijumaa iliyoswaliwa hapa Tehran hii leo ameashiria jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza na kusema kuwa, hadithi ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu, itakuwa hadithi tofauti kabisa kutokana na hamasa na wingi wa watu watakaoshiriki matembezi ya siku hiyo.
Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami amesema hayo leo katika hotuba zake za Swala ya Ijumaa hapa Tehran na kueleza kuwa, Siku ya Kimataifa ya Quds ni kumbukumbu ya Imam Khomeini (MA) na nembo ya kuwa hai tafa la Kiislamu la Iran.
Ameeleza bayana kuwa, hakuna shaka pia mwaka huu wananchi wa Iran watashiriki kwa hamasa kubwa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds kwa sababu tukio hili lina umuhimu maalumu kwao na litapelekea kudhoofika utawala haramu wa Israel ambao unaelekea kusambaratika.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amebainisha kuwa, maandamano ya Siku ya Quds yanakumbusha wajibu wa kumsaidia madhulumu na kupinga dhulma; na kutekeleza wajibu huo ndio kutetekeleza kivitendo nara ya "Mauti kwa Israel."
Aidha Ayatullah Khatami amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa imethibitisha kwamba safu ya kambi ya muqawama imeshikamana barabara, na kwamba utawala wa Kizayuni unajaribu kuihadaa dunia kuwa haujafeli, lakini umeshindwa kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia ya miaka 76 ya utawala huo.
Ayatullah Khatami ameashiria katika sehemu nyingine ya hotuba zake juu ya shambulizi la kigaidi la hivi karibuni katika mji mkuu wa Russia, Moscow na kusema kuwa: Tunalaani ugaidi katika sehemu yoyote ile duniani. ISIS si chochote isipokuwa zao la Marekani.
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesisitiza kuwa, kundi la kigaidi la ISIS (Daesh) lililotagaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi ya Russia iliyoua watu zaidi ya 140 ni shirika Marekani na utawala wa Kizayuni.