Aliyeongoza mashambulizi ya kigaidi kusini mashariki mwa Iran, atiwa mbaroni
(last modified Sat, 06 Apr 2024 10:35:22 GMT )
Apr 06, 2024 10:35 UTC
  • Aliyeongoza mashambulizi ya kigaidi kusini mashariki mwa Iran, atiwa mbaroni

Msemaji wa Komandi Kuu ya Jeshi la Polisi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza habari ya kutiwa mbaroni gaidi aliyeongoza mashambulizi ya kigaidi huko kusini mashariki mwa Iran. Gaidi huyo ametiwa mbaroni kwenye mji wa Karaj wa mkoa wa Alborz wa magharibi mwa Tehran.

Shirika la habari la IRIB limemnukuu Said Montazer Al-Mahdi, Msemaji wa Jeshi la Polisi la Iran akisema leo Jumamosi kwamba, gaidi huyo aliyetiwa mbaroni anajulikana kwa jina la Mohammad Zaker maarufu kwa jina la Ramesh. Ni miongoni mwa walioongoza timu ya operesheni ya kigaidi katika mkoa wa Sistan na Baluchistan wa kusini mashariki mwa Iran. 

Ametoa ufafanuzi zaidi kwa kusema, gaidi huyo ametiwa mbaroni pamoja na magaidi wengine katika mji wa Karaj ambao ni makao makuu ya mkoa wa Alborz wa magharibi mwa Tehran na wamewekwa nguvuni katika operesheni maalumu ya maafisa wa kulinda usalama wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wametiwa mbaroni baada ya gari waliokuwa wanasafiria kupigwa risasi na kujeruhiwa watu watatu waliokuwemo kwenye gari hiyo.

Said Montazer Al-Mahdi, Msemaji wa Jeshi la Polisi la Iran

 

Msemaji wa Jeshi la Polisi la Iran ameongeza kwamba, magaidi hao walikuwa wanapanga njama za kufanya mashambuliizi mengine ya kigaidi wakati wa sikukuu ya Idul Fitr hapa Iran.

Vilevile amesema, sambamba na kutiwa mbaroni magaidi hao, magaidi wengine wanane wametiwa mbaroni wakihusishwa na vitendo vya kigaidi humu nchini na taarifa zaidi kuhusu operesheni za kutiwa nguvuni magaidi hao zitatolewa katika siku zijazo.