Apr 18, 2024 07:31 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu iliikuwa imeshaitaarifu serikali ya Marekani kabla ya kutekeleza Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya kuutia adabu utawala wa Israel mfanyamauaji ya kimbari.


Kwa mujibu wa IRNA, Hossein Amir-Abdollahian, ameyasema hayo mara baada ya kuwasili mjini New York, alipozungumzia Operesheni ya Ahadi ya Kweli ya kuutia adabu utawala wa Kizayuni kwa sababu ya jinai uliyofanya ya kushambulia sehemu ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.

Amir-Abdollahian amekosoa upuuzaji uliofanywa na Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama wa kutolaani jinai hiyo na akasema, tangu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilipoamua kujibu mapigo yanayohitajika ya kuutia adabu utawala wa Israel kulingana na sheria za kimataifa na haki ya Uhalali wa Kujihami, serikali ya Marekani ilifahamishwa juuu ya suala hilo.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, baada ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli Marekani ilifikishiwa salamu nyingine kupitia njia za kidiplomasia na ikatangazwa kinagaubaga na kwa wazi kwamba Iran haina nia ya kupanua mivutano katika eneo na kwamba kinachoweza kusababisha kuongezeka mivutano katika eneo ni mwenendo utakaoonyeshwa na utawala wa Kizayuni.

Amir-Abdollahian aidha amesema kuhusu madhumuni ya safari yake ya mjini New York ya kwamba, katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kitakachojikita kuchunguza matukio ya Asia Magharibi na suala la Palestina, mitazamo ya Iran itabainishwa kuhusiana na ulazima wa kuimarisha amani na usalama endelevu katika eneo na kufanyika mashauriano kwa ajili ya kusitishwa vita mara moja katika Ukanda wa Ghaza, kupelekwa misaada ya kibinadamu kwa wingi katika eneo hilo pamoja na masuala mengine yanayohusiana na kadhia ya Palestina na usalama wa eneo.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwasili katika uwanja wa ndege wa John F. Kennedy mjini New York jana Jumatano kushiriki katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.../

 

Tags