Apr 19, 2024 07:58 UTC
  • Vyombo vya habari: Iran imetungua ndege tatu zisizo na rubani katika mji wa Esfahan

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran umetungua ndege tatu ndogo zisizo na rubani katika mkoa wa Esfahan ulioko katikati mwa nchi saa kadha baada ya vyombo vya habari vya Marekani kuwanukuu maafisa waandamizi wa nchi hiyo wakidai kwamba makombora ya utawala wa Kizayuni wa Israel yamepiga eneo la Iran.

Hata hivyo vyombo hivyo vya habari vimemnukuu Brigedia Jenerali wa Pili Siavash Mihandoust, afisa mkuu wa kijeshi mkoani Esfahan, akiviambia vyombo vya habari vya hapa nchini kwamba betri za ulinzi wa anga ziligonga "kitu kinachotiliwa shaka" na hakukuwa na uharibifu wowote uliotokea.

Esfahan inachukuliwa kuwa mji muhimu kimkakati ukiwa na vituo muhimu kadhaa, ikiwa ni pamoja na vya utafiti wa kijeshi na vya maendeleo, pamoja na vituo vya kijeshi. Mji wa karibu na mkoa huo wa Natanz ni moja ya maeneo ya kurutubisha urani kwa ajili ya matumizi ya amani ya nyuklia.

Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB limetangaza kuwa, mitambo ya ulinzi wa anga ya miji ya Esfahan na Tabriz iliwashwa kufuatia kuonekana vyombo vidogo kadhaa vya angani na vitu vya kutiliwa shaka.

Licha ya baadhi ya ripoti zilizodai kutokea miripuko katika miji hiyo, vyanzo vya kuaminika vimesema hakuna ripoti kwamba umetokea mripuko au kupigwa kwa kombora.

Taarifa zaidi zimeeleza kuwa hali katika miji hiyo wakati huu ni shwari.../

 

Tags