Apr 24, 2024 12:11 UTC
  • Nasser Kan'ani
    Nasser Kan'ani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa, ukiukaji wa kutisha wa haki ya kupiga kura, uhuru wa kusema na haki za binadamu huko Marekani unawatia wasiwasi mkubwa watu duniani.

Baada ya kupita siku 200 tangu kuanza vita dhidi ya Gaza na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wasio na hatia wa Palestina bila ya kuhukumiwa utawala huo, huku serikali ya Biden ikiuhami kifedha, kijeshi na kisiasa  vyuo vikuu vya Marekani sasa vimekuwa uwanja wa ukandamizaji na vitendo vya mabavu dhidi ya wanafunzi wanaoandamana kupinga mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Kipalestina wa Ukanda wa Gaza.   

Maandamano na mikusanyiko mikubwa ya wanafunzi katika vyuo vikuu vya Marekani yamejiri katika kipindi cha miezi saba iliyopita kupinga jinai za Israel huko Ukanda wa Gaza hususan mauaji ya kimbari, na hatua ya utawala wa Kizayuni ya  kutumia silaha ya njaa katika eneo hili dhidi ya Wapalestina. Maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Marekani yanafanyika ili kutaka kusitishwa haraka mauaji ya kimbari na kuzidishwa misaada ya kibinadamu kwa kwa ajili ya watu wa Gaza.  

Maandamano ya wanavyuo Marekani dhidi ya mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza 

Kwa msingi huo, Nasser Kan'ani msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika leo katika ukurasa wake wa mtandao wa X kwamba: Ripoti za habari kuhusu hatua ya polisi wa Marekani ya kuamiliana kwa mabavu na kuwatia mbaroni wanafunzi wengi wa wa vyuo vikuu nchini humo kwa sababu tu ya kuiunga mkono Palestina ni ukiukaji wa haki za kupiga kura, uhuru wa kujieleza na ni uvunjaji wa haki za binadamu; masuala yanayowatia wasiwasi walimwengu. 

Kanani ameongeza kuwa: Ni muhimu kwa serikali ya Marekani kuheshimu wajibu wake wa kulinda haki za binadamu, kudhamini uhuru wa kujieleza na kuwaruhusu wanafunzi wa vyuo vikuu na wahadhiri wa vyuo hivyo kufanya maandamano na inapasa kuheshimu matakwa na haki zao za kisheria. 

Tags