Apr 28, 2024 04:31 UTC
  • Ukandamizaji hautawanyamazisha waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina nchini Marekani

Uwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva umelaani vikali ukandamizaji unaoendelea dhidi ya waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina katika vyuo vikuu vya Marekani, na kusisitiza kwamba ghasia dhidi ya waandamanaji wa amani hazitawanyamazisha.

Huku Marekani ikilendelea kuunga mkono Israel katika mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza kwa muda wa zaidi ya siku 200, vyuo vikuu vikuu vya Marekani vimekuwa eneo la mapigano kati ya wanafunzi na maafisa wa polisi. Wanafunzi wamejitokeza kwa maelefu katika maandamano ya amani ya kulaani vita vya utawala huo ghasibu dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Wanafunzi na wahadhiri wa vyuo vikuu zaidi ya 20 nchini Marekani wanaandamana takribani kila siku kupinga vita hivyo, ambapo hadi sasa Israel imeua zaidi ya Wapalestina wasiopungua 34,000 tangu Oktoba mwaka jana, wengi wakiwa ni wanawake na watoto.

Wanafunzi hao wanatoa wito kwa vyuo vikuu kujitenga na makampuni yoyote ambayo yanaendeleza vita vya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Gaza. Polisi wamewakamata mamia ya waandamanaji katika kampasi za vyuo vikuu.

Katika taarifa kupitia ukurasa wa X siku ya Jumamosi, Uwakilishi wa Kudumu wa  Iran mjini Geneva umeandika hivi, "Tunalaani vikali ukandamizaji wa kikatili na vurugu dhidi ya maandamano ya amani ya kuunga mkono Wapalestina yaliyoenea katika vyuo vikuu nchini Marekani. Ukatili wa Polisi wa Marekani na matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa mikusanyiko ya amani, na kuwalenga wanafunzi wanaotetea kukomesha vita vya mauaji ya kimbari huko Gaza ni jambo la kutia wasiwasi sana."

"Waandamanaji wanatoa wito wa kukomeshwa ushiriki wa Marekani katika mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza kwa jina lao. Kuwafyatulia risasi na kuwapiga waandamanaji wa amani hakuwanyamazishi, kwani  ni watetezi wa haki za binadamu walio mstari wa mbele. Harakati yao inathibitisha tu udharura wa mapambano ya haki kwa Palestina."

Aidha taarifa hiyo imetoa wito wa kuachiliwa wanafunzi na wahadhiri wote waliokamatwa na polisi wakiwa katika maandamano ya amani kote Marekani.

Utawala wa Marekani umekuwa ukiipatia Israel usaidizi wa kijeshi, kijasusi na kifedha tangu Oktoba 7, wakati utawala huo ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Gaza.