May 29, 2024 03:40 UTC
  • YouTube 'yajigonga' katika dai la uhuru wa maoni kwa kuifunga akaunti ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Mtandao wa kijamii wa YouTube umeifuta akaunti rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran kwa kisingizio cha kukiuka kanuni zake kufuatia hatua ya akaunti hiyo kuweka mkanda wa video wa lugha ya Kiingereza wenye anuani "Resistance, the only option for Palestine", yaani Muqawama ndilo chaguo pekee kwa Palestina.

YouTube imechukua hatua hiyo katika hali ambayo Wamagharibi wamejitambulisha kizandiki kuwa ni watetezi wakubwa kabisa wa uhuru wa kutoa maoni unaotajwa kama msingi mkuu wa demokrasia ya Uliberali.
Ikumbukwe kuwa tangu vilipoanza vita vya kidhalimu vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Ghaza, mitandao ya kijamii ya Marekani na Magharibi, imekuwa ikitumia visingizio hewa na vya uongo vinavyogongana waziwazi na uhuru wa kutoa maoni ili kuzifuta au kuziwekea vizuizi na mipaka akaunti za watu binafsi, taasisi au makundi yanayoweka hadharani jinai za kinyama zinazofanywa na Israel huko Ghaza.

 

Jumapili usiku, jeshi la utawala ghasibu wa Israel lilishambulia kwa makombora kambi ya wakimbizi katika mji wa Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza na kuwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 45 wakiwemo wanawake na watoto na kujeruhi wengine 249.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Palestina, karibu nusu ya watu waliouawa shahidi katika shambulio hilo la kinyama walikuwa wanawake, watoto na wazee.
Katika taarifa tofauti, Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Palestina za Hamas na Jihadul-Islami zimetoa tamko kuhusiana na mauaji yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo la kaskazini magharibi mwa mji wa Rafah na kueleza kwamba jinai hiyo ni ithibati ya wazi ya kudharau na kudunisha hukumu iliyotolewa hivi karibuni na Mahakama ya Kimataifa ya kutaka kusimamishwa mara moja mashambulio dhidi ya mji huo. Taarifa za harakati hizo za ukombozi wa Palestina zimesisitiza kuwa serikali ya Marekani na rais mwenyewe wa nchi hiyo Joe Biden ndio wanaobeba dhima ya jinai hiyo ya Rafah.../
 

 

Tags