Iran: Marekani na Israel lazima ziwajibishwe kwa mauaji ya kimbari ya Ghaza
(last modified Mon, 10 Jun 2024 08:07:16 GMT )
Jun 10, 2024 08:07 UTC
  • Iran: Marekani na Israel lazima ziwajibishwe kwa mauaji ya kimbari ya Ghaza

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel zimeshindwa katika vita vyao dhidi ya Ukanda wa Ghaza uliozingirwa na lazima ziwajibishwe kwa mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.

Akizungumza na waandishi wa habari na wasimamizi wa vyombo vya habari siku ya Jumapili, Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema Marekani inashiriki katika jinai za utawala wa Israel dhidi ya Wapalestina huko Ghaza kwa kuipatia uungaji mkono kamili.
 
Kan'ani ameongezea kwa kusema: "Utawala wa Kizayuni, kwa uwezo wake wote wa kijeshi na ushawishi wake wa kisiasa, umeshindwa katika medani ya vita dhidi ya watu wa Palestina".
 
Amesisitiza kuwa: aliyeshindwa zaidi katika vita dhidi ya watu wa Ghaza, mbali na utawala ghasibu wa Kizayuni, ni serikali ya Marekani.
Moja ya usaidizi wa US kwa Israel ni kupigia veto maazimio ya UN ya kusitisha vita Ghaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa, mataifa na serikali za dunia zina wajibu wa kuiwajibisha serikali ya Marekani kwa kutoa uungaji mkono kamili na usio na masharti kwa utawala wa Kizayuni.

Kan'ani ameashiria jukumu muhimu ambalo mataifa ya ulimwengu yanaweza kutekeleza katika kuiwajibisha Israel kwa jinai zake dhidi ya Wapalestina.

Amebainisha kuwa vyombo vya habari vinaweza pia kutoa mchango mkubwa na muhimu katika uungaji mkono wa mataifa ya dunia kwa Wapalestina.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameuelezea uungaji mkono kwa watu wanaodhulumiwa wa Palestina kama "wajibu wa kimataifa" na akasema, makundi ya Muqawama katika eneo yameonyesha azma yao thabiti katika suala hilo.

Wapalestina wasiopungua 37,084 wameuawa shahidi, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto na wengine 84,494 wamejeruhiwa hadi sasa katika mashambulizi ya kinyama yaliyoanza kufanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza tangu tarehe 7 Oktoba 2023.../.../