Iran: Nchi za Magharibi zimepoteza utu na heshima katika vita vya Gaza
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, nchi za Magharibi zimepoteza utu na heshima yao katika vita dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na zimekumbwa na mmomonyoko wa kimaadili na mporomoko wa ustaarabu.
Nasser Kan'ani ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba" "Katika kamusi ya Marekani na nchi za Ulaya, watu na makundi yanayotetea ardhi yao dhidi ya majeshi ya kigeni na yanayopigana na jeshi vamizi, lililojizatiti kwa silaha na linaloua watoto na wanawake, kwa ajili ya kulinda makazi yao, familia na binadamu, yanatambuliwa kuwa ni magaidi.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameongeza kuwa: "Upande wowote unaotetea na kuunga mkono taifa linalodhulumiwa na lililochini ya uvamizi la Palestina, unatambuliwa kuwa ni muunga mkono wa ugaidi; Lakini utawala ghasibu (Israel) uliuoua watu zaidi ya 40,000 ndani ya miezi 10, zaidi ya 10,000 kati yao wakiwa watoto, si tu kwamba sio utawala wa kigaidi, bali pia unastahili kutiwa moyo na kupewa misaada ya aina mbalimbali ya kisiasa, kiusalama, kijeshi na silaha!!!"
Licha ya upinzani wa kieneo na kimataifa, utawala bandia wa Israel unaendelea kushambulia watu wa Ukanda wa Gaza tangu miezi 10 iliyopita, na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi ndizo wafadhili wakubwa wa silaha na misaada ya kijeshi kwa utawala huo wa kihalifu.