Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alihimiza taifa la Iran kusimama kidete katika vita vya kisaikolojia vya adui
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, amezungumzia hila na njama za wasiolitakia mema taifa la Iran katika kuanzisha vita vya kisaikolojia na kutaka kulirudisha nyuma katika nyuga mbalimbali na kusema, utambuzi wa uwezo wa ndani na kuepuka kutia chumvi nguvu za maadui ndiyo njia pekee ya kukabiliana na njama hizo.
Ayatullah Khamenei aliyasema hayo jana (Jumatano) alipokutana na wajumbe wa Kongamano la Kitaifa la Mashahidi wa Mkoa wa Kohgiluyeh na Boyer-Ahmad, na kuongeza kuwa, moja ya misingi mikuu ya vita vya kisaikolojia dhidi ya taifa la Iran ni kukuza na kutilia chumvi uwezo wa maadui. Amesema, lengo la vita vya kisaikolojia vya adui katika nyuga mbalimbali hususan za kijeshi ni kuzusha hofu na kuridisha nyuma taifa la Iran kutokana na mafanikio yake, lakini njama hizo zimefeli kutokana na kuwa macho na makini kwa taifa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kazi kubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kuondoa woga katika nyoyo za taifa na kuzidisha hali ya kujiamini. Ameongeza kuwa: "Taifa letu linahisi kwamba lina uwezo wa kufanya mambo makubwa kwa kutegemea nguvu zake za ndani; na adui hana nguvu kubwa kama anavyojidhihirisha."
Vita vikubwa vya kinafsi na vya vyombo vya habari ambavyo vimeshadidi dhidi ya Iran katika siku hizi vikiongozwa na Marekani, vinalenga kuzua mkwamo katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ili kuwafanya watu wa Iran waamini kuwa mfumo wa Kiislamu haufai tena. Msisitizo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu udharura wa kuwa macho taifa la Iran dhidi ya vita vya kisaikolojia vya adui, umetolewa wakati Marekani na waitifaki wake wa Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel, wakiwa wameanzisha vita vya kisaikolojia vya kila upande dhidi ya Iran katika miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya duru mpya ya mauaji ya Wazayuni huko Gaza, kutokana na uungaji mkono wa Tehran kwa Muqawama wa watu wa Palestina ili kueneza hali ya kukosa matumaini na kukata tamaa katika jamii ya Iran. Hatua ya sasa ya Marekani ya kupeleka majeshi yake katika eneo la Magharibi mwa Asia, kuzidishwa vitisho vya utawala wa Kizayuni wa Israel, na kueneza taswira mbaya kuhusu hali ya ndani ya Iran katika fikra za wananchi, ni miongoni mwa hatua ambazo Marekani na waitifaki wake wameziweka kwenye ajenda yao katika duru mpya ya vita vya kisaikolojia na kipropaganda dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa uungaji mkono wa wananchi, haijaacha kujibu vitisho na mashambulizi yoyote dhidi ya maslahi yake ndani na nje ya mipaka, kama iliyokuwa siku zote. Shambulio la Iran ambalo halijawahi kushuhudiwa katika kambi ya kijeshi ya Marekani nchini Iraq baada ya mauaji ya kigaidi ya Shahidi Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na shambulio la hivi karibuni la makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya kambi za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya jeshi la utawala huo kushambulio ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, vinatathminiwa katika mwelekeo huo.
Ni katika fremu hiyo ambapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akasema hisia za udhaifu, kutengwa na kusalimu amri mbele ya matakwa ya maadui ni miongoni mwa taathira za kukuza na kutilia chumvi nguvu za maadui katika uga wa kisiasa, na kusisitizia kwamba, iwapo serikali zitasimama imara dhidi ya matakwa ya mabeberu kwa uungaji mkono wa wananchi, hapana shaka kuwa zitaweza kuzima njama zao hususan, vita vya kinafsi na kisaikolojia.
Kusimama imara na umoja wa wananchi na taasisi zote ndio ufunguo na siri ya mafanikio ya Iran katika kukabiliana na njama za aina mbalimbali. Kwa hivyo, hii leo pia katika vita vya kisaikolojia vya pande zote vya adui, inatarajiwa kwamba Iran itavuka vigingi hivyo kwa kubuni sera sahihi na makini. Katika muktadha huu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, iwapo tutaendelea kusimama kidete kukabiliana na maadui, watalazimika kurudi nyuma, na hatimaye taifa la Iran litapata ushindi kwa msaada wa Mwenyezi Mungu.