Iran: Hatuna nafasi yoyote katika vita vya Russia na Ukraine
(last modified Sun, 08 Sep 2024 12:04:19 GMT )
Sep 08, 2024 12:04 UTC
  • Iran: Hatuna nafasi yoyote katika vita vya Russia na Ukraine

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haina mchango wowote katika vita vinavyoendelea kati ya Russia na Ukraine, na daima imekuwa ikikariri wito wake wa mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo huo.

Nasser Kan'ani amesema hayo leo Jumapili, siku moja baada ya vyombo vya habari vya Marekani vikinukuu vyanzo visivyojulikana kudai kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imeipelekea Russia makombora ya masafa mafupi ya balistiki.

Kan'ani amesisitiza kwamba, mtazamo wa Tehran kuhusu mgogoro wa Ukraine bado "haujabadilika" na kwamba madai hayo "yasiyo na msingi kabisa" kuhusu kupelekwa makombora ya balistiki ya Iran huko Russia yanaoana na malengo ya kisiasa ya baadhi ya nchi za Magharibi.

Halikadhalika, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amepuuzilia mbali madai kwamba mwanajeshi wa Jamhuri ya Kiislamu amekuwa akitoa mafunzo kwa wanajeshi wa Russia katika ardhi ya Ukraine.

Amebainisha kuwa Iran haiungi mkono vita akisisitiza haja ya kusimamishwa mgogoro huo na kutatua mizozo kati ya Russia na Ukraine kwa njia ya amani.

Kan’ani ameongeza kuwa, kinachoshuhudia nchini Ukraine ni matokeo ya sera na vitendo vya kichochezi vya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani.

Huko nyuma pia, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran alisema kuwa, madai ya Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi NATO kwamba Iran inaisadia kijeshi Russia katika vita vya Ukraine hayana msingi wowote.