Iran yalaani shambulio la Israel dhidi ya skuli ya UN Gaza
(last modified Fri, 13 Sep 2024 03:05:56 GMT )
Sep 13, 2024 03:05 UTC
  • Iran yalaani shambulio la Israel dhidi ya skuli ya UN Gaza

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani shambulizi la anga la Israel dhidi ya shule nyingine iliyogeuzwa makazi na wakimbizi katika Ukanda wa Gaza, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 18, wakiwemo wafanyakazi sita wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA).

Katika taarifa aliyoituma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X jana Alhamisi, Nasser Kan’ani alisema shule na mahema ya wakimbizi katika Ukanda wa Gaza ndiyo shabaha kuu ya hujuma za kila siku za utawala katili wa Israel.

Amezikosoa vikali Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Canada na Australia kwa kuipatia Israel makombora inayoyatumia dhidi ya watu wa Palestina.

Vikosi vya jeshi la Israel siku ya Jumatano vilishambulia shule ya al-Jawni katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza inayowahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao kwa mara ya tano katika miezi zaidi ya 11 ya vita.

Mashuhuda wa shambulio hilo la kinyama la Jumatano wamesema "wanawake na watoto waliripuliwa na kukatika vipande vipande" katika hujuma hiyo.

Nasser Kan’ani

Akizungumzia shambulio hilo katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema: "kinachotokea Gaza hakikubaliki hata kidogo.

Guterres amebainisha kuwa, "Skuli iliyogeuzwa makazi ya takribani watu 12,000 imeshambuliwa tena na Israel; wenzetu sita wa UNRWA ni miongoni mwa waliouawa."