Iran yauandikia barua muhimu Umoja wa Mataifa na kutoa onyo kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel
-
Amir Saeed Iravani
Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amemwandikia barua Katibu Mkuu na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo kufuatia operesheni ya makombora iliyofanywa na Iran, na kusisitiza kuwa, endapo utawala wa Israel utarudia tena vitendo vyake vinavyokiuka sheria za kimataifa, jibu litakalotolewa tena na Iran litakuwa la haraka, madhubiti na kali zaidi kuliko lililiotangulia.
Katika barua yake hiyo, Amir Saeed Iravani amesema: "kufuatia agizo la serikali yangu na baada ya barua ya tarehe 31 Julai, 2024 (S/2024/584), ningependa kukujulisha Mheshimiwa na wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba, jioni ya Jumanne, Oktoba 1, 2024 (kwa saa za eneo letu) Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilifanya mashambulizi ya mfululizo ya makombora dhidi ya maeneo ya kijeshi na usalama ya utawala wa Israel".
Imeelezwa katika barua hiyo: "hatua hii inaendana na haki ya dhati ya kujilinda, kulingana na Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa, na kwa ajili ya kujibu vitendo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni, ikiwa ni pamoja na kukiuka mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa Hamas ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani wa Palestina yaliyofanywa Tehran Julai 31, 2024, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa serikali ya Iran; kujeruhiwa balozi wa Iran nchini Lebanon kutokana na kulengwa makusudi na kiholela raia nchini Lebanon mnamo Septemba 17, 2024 kupitia uripuaji wa pager; mauaji ya Katibu Mkuu wa Hizbullah huko Lebanon na Kamanda Abbas Nilfroushan, Mshauri Mwandamizi wa kijeshi wa Iran mjini Beirut".

Sehemu nyingine ya barua ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imesema: "tofauti na utawala wa Kizayuni, ambao ungali unaendelea kuwachukulia raia wasio na hatia na miundombinu ya kiraia kuwa ni shabaha na walengwa halali wa hujuma na mauaji ya halaiki, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa kuzingatia misingi ya kimaadili na mafundisho matukufu ya Uislamu na kwa kuchunga kikamilifu msingi wa upambanuzi katika sheria za kimataifa za kibinadamu, imezilenga taasisi za kijeshi tu na kiusalama za utawala huo katika mashambulizi yake ya makombora ya kujilinda".
Iravani ameendelea kubainisha katika barua hiyo: "ni jambo la kusikitisha kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kimsingi na muhimu wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa. Kutochukua hatua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kumeupa idhini utawala ghasibu wa Israel ya kuivuka wazi wazi mistari yote myekundu na kukiuka misingi mikuu ya sheria za kimataifa zikiwemo sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu za kimataifa.
Katika barua yake hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Iran UN ameongezea kwa kusema: "kufeli huku kumeilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutumia haki zake za kisheria kwa mujibu wa sheria za kimataifa na kuchukua hatua za kisheria kulinda usalama wake wa taifa na maslahi yake muhimu".

Barua hiyo imetanabahisha pia kwa kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa onyo kali dhidi ya hatua zozote za kichokozi za utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya usalama wake wa taifa na maslahi yake muhimu". Barua hiyo ya balozi wa Iran imesema: "Iran imejiandaa kikamilifu ili pale itapolazimu, kuchukua hatua zaidi za kiulinzi, kwa ajili ya kulinda maslahi yake halali, mamlaka yake na umoja wa ardhi yake dhidi ya uvamizi na uchokozi wowote wa kijeshi na matumizi haramu ya nguvu. Endapo utawala wa Israel utarudia tena hatua za aina hii zinazokiuka sheria za kimataifa, jibu la Iran litakuwa la haraka, madhubuti na kali zaidi kuliko lililotangulia. Iran haitasita hata kidogo kuhusiana na hili.../