Cairo, hatua ya nane ya safari ya kieneo ya Araghchi
(last modified 2024-10-18T02:50:03+00:00 )
Oct 18, 2024 02:50 UTC
  • Cairo, hatua ya nane ya safari ya kieneo ya Araghchi

Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Cairo, mji mkuu wa Misri, katika kituo cha nane cha safari yake ya kieneo ambapo amekutana na kuzungumza na rais na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa nchi hiyo.

Vita katika eneo hili nyeti la Asia Magharibi vimechukua mkondo mpya wenye kasi kubwa. Utawala wa Kizayuni unaendelea kufanya jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza, na wakati huo huo kueneza jinai zake dhidi ya Lebanon ambapo unajaribu kuuharibu mji  Beirut kwa mabonu yenye nguvu kubwa kama ulivyofanya huko Gaza. Wakati huo huo utawala wa Kizayuni ambao baada ya kumuua kigaidi Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na Meja Jenerali Nilfroushan, mshauri wa masuala ya kijeshi wa Iran nchini Lebanon, ulikabiliwa na operesheni kali ya Ahadi ya Kweli nambari 2 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, sasa unajaribu kupanua vita katika nchi kadhaa za Asia Magharibi.

Kuhusiana na hilo, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya safari za kieneo kwa shabaha ya kuzuia kuenea vita na kuonya dhidi ya madhara yake katika eneo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, ambaye awali alisafiri katika nchi za Lebanon, Syria, Saudi Arabia, Qatar, Iraq, Oman na Jordan, amekwenda Cairo katika ziara yake ya nane kieneo ambapo amekutana na kushauriana na Rais Abdel Fattah Sisi na Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri. Safari ya Araghchi nchini humo ni muhimu zaidi kuliko safari zake katika mataifa mengine ya eneo.

Araghchi (kushoto) alipokutana na Rais Abdulfattah As-Sisi mjini Cairo

Sababu ya kwanza ni kuwa safari ya Araghchi huko Misri imefanyika baada ya miaka 12 na kufuatia safari ya mawaziri wawili wa mambo ya nje wa Misri mjini Tehran kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya kuwaenzi Mashahidi wa ndege ya Mwezi Mei na kukutana na Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na vilevile baada ya  mawasiliano na mikutano kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizi mbili baada ya mkutano wa Shahidi Sayyid Ebrahim Raisi na Abdul Fattah Al-Sisi, marais wa nchi mbili, pembeni ya Mkutano wa Kilele wa Ushirikiano wa Kiislamu mjini Riyadh mwanzoni mwa mwaka huu. Kwa hiyo, nchi mbili hizi ambazo hazina uhusiano wa kidiplomasia katika ngazi ya juu na zina ofisi tu za kulinda maslahi ya pande mbili, zimechukua hatua muhimu za kupanua mahusiano yao.

Sababu ya pili ni kwamba, Misri ina nafasi maalum katika mgogoro kati ya Palestina na utawala wa Kizayuni. Misri imekuwa na nafasi kongwe na yenye ushawishi mkubwa katika mzozo wa Waarabu na utawala wa Israel. Hivi sasa pia, Misri na Qatar ni nchi mbili za Kiarabu ambazo zina nafasi muhimu katika diplomasia hai ya kumaliza vita huko Gaza. Mazungumzo ya kumaliza vita vya Gaza yamekuwa yakifanyika kwa kuwashirikisha wajumbe wa Israel, Marekani, Misri na Qatar. Kwa hivyo, safari ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran mjini Cairo ina umuhimu maalum kwa kutilia maanani nafasi muhimu na yenye taathira ya Misri katika uga wa matukio ya eneo hususan kadhia ya Palestina. Katika hali hiyo, Badr Abdelatty Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, amesema kuwa, safari ya Araghchi mjini Cairo ni katika mwelekeo wa juhudi za Misri za kupunguza mivutano katika eneo.

Abdallah al-Ash'al, naibu waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Misri ameliambia gazeti la al-Arabi al-Jadeed kwamba Iran inaipa umuhimu mkubwa Misri, na hili linatokana na nafasi yake katika eneo, hasa katika mazungumzo na juhudi zinazohusiana na usitishaji vita, katika mwaka mmoja uliopita kati ya muqawama wa Wapalestina huko Gaza na utawala ghasibu wa Israel. Kutokana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya utawala wa Israel na Misri, Cairo inataka kuwa na nafasi athirifu katika kupunguza mvutano kati ya Iran na utawala huo.