Iran yaonya kuhusu 'ushiriki hatari' wa Marekani na Uingereza katika chokochoko za Israel
(last modified 2024-10-19T11:31:35+00:00 )
Oct 19, 2024 11:31 UTC
  • Iran yaonya kuhusu 'ushiriki hatari' wa Marekani na Uingereza katika chokochoko za Israel

Iran imelaani vikali mashambulizi ya anga ya pamoja ya Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen huku nchi hizo mbili zikiunga mkono utawala haramu wa Israel kijeshi na kisiasa.

Msemaj wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei amesema mashambulizi hayo dhidi ya Yemen yanathibitisha ushiriki wa Uingereza na Marekani katika ukatili wa utawala wa Kizayuni.

Aidha amesema mashambulio ya mapema Alhamisi dhidi ya maeneo ya San'an na Sa'ada nchini Yemen ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa kuhusu marufuku ya matumizi ya nguvu na ulazima wa kuheshimu mamlaka ya kujitawala nchi.

Baghaei amesema: "Uchokozi wa Marekani na Uingereza dhidi ya watu wanaodhulumiwa na shupavu wa Yemen ni sawa na ushiriki hatari wa nchi hizi mbili katika kushadidisha hali ya ukosefu wa usalama na mivutano katika eneo la Asia Magharibi, jambo ambalo linauchochea utawala wa Israel kuendelea na mauaji ya kimbari na sera zake za kivita."

Baghaei amepongeza "uungaji mkono wenye heshima" wa Wayemen kwa mataifa yanayodhulumiwa ya Palestina na Lebanon, akisema mshikamano wa taifa la Yemen na watu wa Palestina na Lebanon hauwezi kudhoofishwa kwa mashambulizi na uharibifu wa miundombinu muhimu ya nchi hiyo.

Msemaj wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei 

 

Siku ya Alhamisi ndege za kivita za Marekani na Uingereza zilishambulia kwa mabomu mji mkuu wa Yemen, Sana'a na maeneo mengine kadhaa, huku Wizara ya Ulinzi ya Marekani ikijigamba kuwa  ilitumia ndege zisizoonekana kwenye rada za B-2 kwa mara ya kwanza katika mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen.

Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen Abul-Malik al-Houthi akizungumza baada ya hujuma hiyo ya Marekani na Uingereza ameisema mashambulizi hayo hayatazuia Yemen kuendelea na operesheni zake dhidi ya Israel na washirika wake katika kuunga mkono mataifa ya Palestina na Lebanon.

Wananchi wa Yemen wametangaza uungaji mkono wao wa wazi kwa mapambano ya Palestina dhidi ya uvamizi wa Israel tangu utawala huo ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, 2023.

Vikosi vya jeshi la Yemen vimesema havitasimamisha mashambulizi dhidi ya Israel hadi utawala huo utakapositisha mashambulizi yake dhidi ya Palestina na Lebanon.