Al-Arabi al-Jadid: Kuna uwezekano marais wa Iran na Misri wakaonana karibuni hivi
(last modified 2024-10-20T10:33:28+00:00 )
Oct 20, 2024 10:33 UTC
  • Al-Arabi al-Jadid: Kuna uwezekano marais wa Iran na Misri wakaonana karibuni hivi

Chombo kimoja cha habari cha nchini Qatar kimenukuu duru zake na kusema kuwa, kuna uwezekano marais wa Iran na Misri wakaonana karibuni hivi.

Shirika la habari la FARS limelinukuu gazeti la al Arabi al Jadid likiandika hayo katika toleo lake la leo Jumapili na kuongeza kuwa, hatua za kufanikisha mazungumzo ya ana kwa ana baina ya Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na rais mwenzake wa Misri, Abdel Fattah el Sisi zimeshachukuliwa.

Kwa mujibu wa chombo hicho cha habari cha Qatar, mazungumzo hayo yatafanyika pambizoni mwa mazungumzo ya wakuu wa kundi la BRICS huko Kazan Russia baina ya tarehe 22 hadi tarehe 24 Oktoba yaani kuanzia Jumanne hadi Ijumaa.

Gazeti hilo la nchini Qatar limenukuu wanadiplomasia kadhaa wa Misri ambao haikuwataja majina wakisema hayoi na kuongeza kuwa, katika safari yake ya wiki iliyopita mjini Cairo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifikia makubaliano na viongozi wa Misri kuhusu suala hilo.

Taarifa hiyo imetangazwa katika hali ambayo wizara za mambo ya nje za Iran na Misri zilikuwa hazijasema chochote kuhusu suala hilo hadi wakati tunaandaa taarifa hii.

Ofisi ya Rais wa Iran imetangaza kuwa, Rais Masoud Pezeshkian atahutubia kikao cha 16 cha wakuu wa kundi la BRICS na BRICS Plus Jumanne wiki hii nchini Russia ambacho kitahudhuriwa pia na Rais Abdelfattah el Sisi wa Misri.