Iran ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika teknolojia ya nyuklia
(last modified Mon, 04 Nov 2024 02:23:55 GMT )
Nov 04, 2024 02:23 UTC
  • Iran ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani katika teknolojia ya nyuklia

Kutokana na juhudi za wanasayansi na wataalamu wake vijana, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivi sasa ni miongoni mwa nchi zinazoongoza duniani kwa teknolojia ya nyuklia.

Maendeleo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miaka ya hivi karibuni yamefikia kiwango kikubwa katika nyanja za teknolojia mpya na sasa yanalingana na viwango vya juu kimataifa. Teknolojia ya nyuklia ya Iran pia imepata mafanikio makubwa katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, dawa, uzalishaji umeme na nyanja mbalimbali za kisayansi na matibabu kwa kuzalisha bidhaa tofauti bila ya kutegemea makampuni ya nchi za Magharibi.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi zinazoongoza katika teknolojia ya nyuklia duniani

Kufanyika maonyesho ya teknolojia ya kisayansi katika sehemu mbalimbali za dunia ni fursa nzuri kwa makundi ya kisayansi, wanasayansi vijana na wataalamu wa Iran kuonyesha mafanikio na bidhaa zao katika soko la kimataifa. Suala muhimu la uwepo wa makampuni yenye msingi wa maarifa ya Iran katika maonyesho hayo ni kukiri wasomi, wanasayansi na wajuzi wa mambo kuhusu maendeleo makubwa iliyoyafikia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika sekta ya nyuklia.

Maendeleo hayo yamepatikana katika hali ambayo Marekani na serikali za Magharibi zimekuwa zikiiwekea Iran vikwazo vya kila namna vya teknolojia ya nyuklia yenye malengo ya amani kwa visingizio tofauti vizivyo na msingi, vikwazo ambavyo vingali vinaendelea hadi leo. Marekani na waungaji mkono wake wa Magharibi wameiwekea vikwazo vikali sekta ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani katika hali ambayo utawala wa Kizayuni ambao ni mshirika wao mkuu, umekuwa chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama na amani katika eneo kwa kujizatiti kwa silaha za nyuklia ambazo umezipata kwa msaada wa nchi za Magharibi.

Katika mkutano wake wa hivi karibuni na wanafunzi na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Shiraz, Mohammad Eslami, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kama ninavyomnukuu: "Tumefanikiwa kupata misimbo ya kimahesabu na programu zinazotumika katika mchakato wa kubuni na ujenzi. Misimbo hii hutumika katika utengenezaji wa bidhaa. Kutokana na kuwa Taasisi ya Nyuklia ya Iran ilikuwa imefungiwa milango yote ya kupata misimbo hii, hatukuweza kunufaika nayo, au hatukuweza kuiamini kutokana na uharibifu ambao ungeweza kufanywa na maadui. Kwa hivyo tumeweza kufikia teknolojia hii katika uwanja huu kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na vijana wa sekta ya nyuklia ya Iran." Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kwa kusema: "Katika miaka ya hivi karibuni, Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran imevuka hatua ya utafiti na kuingia katika hatua ya kiviwanda, ambayo tunaendelea kuiimarisha."

Mohammad Eslami, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Maendeleo ya kisayansi na uwezo mkubwa katika uwanja wa teknolojia ya nyuklia, yamepatikana kutokana na juhudi za wanasayansi vijana wa Iran ambao wamefanikiwa kupata misimbo ya kompyuta na programu zinazotumika katika mchakato wa kubuni na kutengeneza bidhaa mbalimbali katika sekta ya nyuklia. Hii ni hatua muhimu sana ambayo inaiwezesha nchi kukamilisha mchakato wa kutenegeneza bidhaa muhimu katika sekta ya nyuklia na kujitosheleza katika uzalishaji wa teknolojia nyeti na muhimu katika sekta hii.

Kufikiwa mafanikio haya ya kisayansi na kiteknolojia nchini Iran, yanatokana na kujiamini na kutegemea uwezo wa ndani ya nchi, na mchakato huu ni matokeo ya azma thabiti na jitihada zisizo na kikomo za vituo vya kielimu na kiutafiti nchini. Maendeleo haya makubwa ya sekta ya nyuklia ya Iran yamepatikana katika miaka ya hivi karibuni huku kukiwa na usimamizi mkali wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na utekelezaji wa protokali ziada ya taasisi hii.

Licha ya uvunjaji ahadi mkubwa wa Marekani na nchi za Magharibi na kukataa nchi hizo kutekeleza majukumu yao kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaendeleza mipango na malengo yake ya amani ya nyuklia na wakati huo huo kuithibitishia jamii ya kimataifa kuwa inaheshimu na kufungamana kikamilifu na ahadi na majukumu yake.

Tags