Waziri wa Mawasiliano wa Iran afanya mazungumzo na Rais wa Venezuela
(last modified Tue, 05 Nov 2024 07:15:28 GMT )
Nov 05, 2024 07:15 UTC
  • Waziri wa Mawasiliano wa Iran afanya mazungumzo na Rais wa Venezuela

Katika siku ya kwanza ya ziara yake nchini Venezuela, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran amekutana na kuzungumza na Rais wa Venezuela.

Sayyid  Sattar Hashemi, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran amekutana na kuzungumza na Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro.

Katika mkutano huo, Maduro amesema, muelekeo wa pamoja uliopo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Venezuela katika nyanja za ustawi na maendeleo ni fursa adhimu na kusisitiza kuwa: sisi tumeungana kwa ajili ya kuleta amani na maendeleo.

Rais wa Venezuela amemhutubu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran akisema: "tumefurahishwa na hatua chanya na za kujenga ulizochukua katika siku kadhaa za kuwepo kwako Venezuela na tuna furaha ya kukukaribisha katika Ikulu ya Rais.

Maduro ameendelea kueleza kwamba amefuraishwa pia na matokeo ya mkutano wake na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran nchini Russia, na  akaongezea kwa kusema: Katika mkutano niliofanya na Rais Masoud Pezeshkian wa Iran mjini Kazani nchini Russia tulisisitiza kuendelezwa ushirikiano wa pamoja na wa kindugu kati ya Iran na Venezuela.

Katika miaka ya hivi karibuni uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi zinazoendelea za Amerika ya Kusini umekuwa ukiongezeka kwa kasi na uhusiano huo umekuwa ukipanuka zaidi  katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kibiashara, kiviwanda, nishati na nyenginezo.