Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina lengo la kumiliki silaha za nyuklia
(last modified Mon, 11 Nov 2024 02:46:08 GMT )
Nov 11, 2024 02:46 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza suala la kujenga hali ya kuaminiana kimataifa na kusema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijawahi kutaka kumiliki silaha za nyuklia na haina lengo hilo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imeripoti kuwa, Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X akisisitiza kuwa Iran haijawahi kutaka kumiliki silaha za nyuklia na haina lengo hilo. "Sera hizi zinatilia maanani mafundisho ya Kiislamu na mahesabu ya kiusalama ya Tehran", amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. 

Araqchi ameeleza kuwa: Kujenga hali ya kuaminiana inapaswa kuwa ya pande zote; na hii si njia ya upande mmoja. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameashiria matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani na kuandika: Wananchi wa Marekani wamefanya uamuzi wao, na Iran inaheshimu haki yao ya kuchagua rais wanayemtaka.