Iran yajibu tuhuma za Katibu Mkuu mpya wa NATO dhidi ya Tehran
(last modified Thu, 05 Dec 2024 11:53:05 GMT )
Dec 05, 2024 11:53 UTC
  • Iran yajibu tuhuma za Katibu Mkuu mpya wa NATO dhidi ya Tehran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekosoa matamshi yaliyotolewa na Katibu Mkuu mpya wa shirika la kijeshi la nchi za Maghjaribi, NATO, akiituhumu Iran kuhusu matukio ya Ukraine na kusema matamshi hayo si ya kuwajibika.

Jumanne iliyopita, Mark Rutte, Katibu Mkuu mpya wa NATO alitoa onyo kwa rais mteule wa Marekani, Donald Trump, akidai kuwa iwapo Ukraine italazimika kulegeza kamba kwa ajili ya kufanya makubaliano ya kusitisha vita na Russia, basi Marekani itakabiliwa na "tishio kubwa" kutoka kwa China, Iran na Korea Kaskazini.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei leo, Alhamisi, amejibu madai ya Katibu Mkuu wa NATO kuhusu amani ya Ukraine kwenye mtandao wa kijamii wa X, akisema kwamba Mark Rutte ambaye anadai kuwa anajua vyema saikolojia ya rais mteule wa Marekani, anang'angania sana kuiainishia majukumu serikali ya baadaye ya Marekani.

Baghaei amekadhibisha tuhuma za Mark Rutte dhidi ya Tehran, akisema kuwa Katibu Mkuu mpya wa NATO anapaswa kushughulikia hali ya ukosefu wa usalama inayozidi kuongezeka dunia ikiwemo huko Ulaya kutokana na siasa za kichochezi na za kiimla za baadhi ya wanachama wa NATO.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amefafanua kuwa agizo la Katibu Mkuu mpya wa NATO si chochote zaidi ya kuhimiza uhasama zaidi kupitia njia ya kuigawa dunia katika kambi mbili; Na mbinu hii isiyofaa ni kielelezo cha kutowajibika.